IQNA

Mawimbi ya Bahari yahatarisha msikiti wa kale Kilifi, Kenya

19:35 - July 15, 2017
Habari ID: 3471068
TEHRAN (IQNA)-Mmoja kati ya misikiti ya kale zaidi nchini Kenya uko katika hatari ya kuangamia kutokana na ongezeko la mawimbi ya bahari.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, msikiti huo, ambao ni mmoja ya vivutio vya magofu ya Jumba La Mtwana katika mji wa Mtwapa ulio katika Kaunti ya Kilifi katika eneo la pwani ya Kenya, unakabiliwa na hatari ya kuangamia kutokana na mawimbi ya bahari kuharibu misingi yake.

Wataalamu wanasema msingi wa msikiti huo unadidimia kutokana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yamepelekea ongezeko la joto duniani hali ambayo imeongeza urefu wa kina cha bahari. Wanaakiolojia wanasema msikiti huo ulijengwa miaka 500 iliyopita.

Gazeti la kila siku la nchini Kenya la Standard limeandika kuwa, wataalamu wa Jumba la Makumbusho ya Kiaifa Kenya wanasema mawimbi makali bahari ya Hindi, yatokanayo na ongezeko la joto duniani, yamepelekea majengo ya kihistoria katika eneo lote la pwani ya Kenya kukabiliwa na hatari ya kuangamia.

Msimamizi wa magofu ya Jumba la Mtwana Hashim Hinzano Mudzomba anasema: "Eneo hili la kihistoria linaangamia kutokana na mabadiliko katika maumbile. Kuna haja ya kuchukua hatua za kurekebisha hali hii ili magofu haya yasiangamie kabisa." Anasema eneo hilo wakati moja lilikuwa kivutio kikubwa kwa watalii wa kitaifa na kignei lakini sasa wamepungua.

Mtaalamu huyo anapendekeza ujenzi wa ukuta wa kuzuia mawimbi ya bahari karibu na magofu yaliyo katika eneo hilo.

Wataalamu wa historia wanasema kuna haja ya hatua za haraka kuchukuliwa kulinda magofu hayo na mengine katika pwani ya Kenya na mwambao wa Afrika Mashariki kwa ujumla kwa sababu maeneo hayo ni utambulisho halisi wa ustaarabu wa Kiswahili na Kiislamu katika eneo hilo.

Mawimbi ya Bahari yahatarisha msikiti wa kale Kilifi, Kenya

3618923

captcha