IQNA

Imam Sadiq AS Mwalimu wa Abu Hanifa na Malik bin Anas

11:48 - July 20, 2017
Habari ID: 3471076
TEHRAN (IQNA)- 25 Shawwal 1438 Hijria inasadifiana na siku ambayo aliuawa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, Imam Jafar Sadiq AS.

Shakhsia huyo mkubwa alikuwa ni taa ya uongofu na mkweli ambaye kwa hakika alikuwa muhimili wa dini katika wakati wake.

Tarehe 25 Shawwal mwaka 148 Hijiria, ulimwengu wa Kiislamu ulipatwa na huzuni kufuatia kuondokewa na mmoja wa Ahlul-Bayti wa Mtume wa Uislamu SAW. Katika siku hiyo, Imam Jafar Swadiq AS akiwa na umri wa miaka 65 aliuawa shahidi kwa amri ya Mansur Dawaaniq, mtawala wa pili wa Bani Abbasi baada ya kupewa sumu.

Makala hii itaangazia kwa kifupi namna imam huyo mtukufu alivyoamiliana na watu akiwa kama marejeo ya Waislamu kutoka makundi yenye fikra na itikadi tofauti katika zama zake.

Maslahi ya Waislamu

Licha ya kwamba Ahlul-Bayti wa Mtume walikabiliwa na changamoto tofauti kisiasa na kijamii, lakini walijitahidi kuhakikisha wanainua bendera ya dini ya Kiislamu katika zama zao zote. Dakta Shahid Mutwahhari, mwanafikra mashuhuri wa Iran anaandika kwa kusema: " Ahlul-Bayti hao walikuwa wakichunga maslahi ya Kiislamu na Waislamu kwa ujumla.

Katika mazingira yote mepesi au magumu, viongozi hao walikuwa wakichunga vivyo hivyo maslahi ya Kiislamu. Aidha katika kila zama viongozi hao walikuwa wakiunda mrengo maalumu wa mapambano, huku wakiupatia elimu kamili mrengo huo ambao ulikuwa na jukumu la kulinda Uislamu."

Moja ya sifa za kipekee za kipindi cha Imam Sadiq ilikuwa ni kuibuka makundi tofauti ya kiitikadi na kisiasa. Suala hilo lilikifanya kipindi cha uimamu wa mtukufu huyo kuwa kipindi muhimu zaidi kati ya vipindi vya maimamu wengine watoharifu katika historia ya Uislamu.

Imam Sadiq AS aliulinda Uislamu

Katika matukio yote hayo, Imam Saadiq AS aliendelea kuulinda Uislamu kwa kuwalea maelfu ya wanafunzi wake kifikra na kitamaduni. Imam alisisitiza juu ya udharura wa kuenezwa mafundisho ya kidini sanjari na kukabiliana na bidaa na fikra zilizo kinyume na Uislamu. Katika harakati hizo, mtukufu huyo alikuwa akibainisha mafundisho na elimu ya Kiislamu kama vile hadithi, fiq'hi, aqida, tafsiri ya Qur'ani na elimu nyenginezo.

Aidha imam alikuwa akiyashawishi makundi mbalimbali ya Waislamu yaliyokuwa na mahusiano naye sambamba na kuwakurubisha karibu yake. Imepokelewa kuwa imam Jafar Sadiq AS alikuwa na mahusiano mema na maulama wa Kisuni pia.

Kwa mtazamo wa imam, farqa, ilikuwa ni chanzo cha kuibua mtetemeko katika ngome ya Uislamu. Ni kwa ajili hiyo ndio maana akawa akiwausia Waislamu hususan wafuasi wake juu ya upendo baina yao wao kwa wao. Kuhusiana na suala hilo anasema:

"Wafikishie salamu wafuasi wetu na wambie kwamba Mwenyezi Mungu anamrehemu mtu ambaye anavutia kwake mapenzi ya watu."

Madhehebu na kuheshimu fikra za wengine

Aidha Imam Sadiq AS alikuwa akiamini kwamba madhehebu na makundi tofauti ya Kiislamu, ni wahusika katika jamii ya Kiislamu na kwamba ni lazima kuheshimu fikra na mrengo wa mwengine. Kwa ajili hiyo Waislamu mbali na kulinda mahusiano na urafiki kati yao, wanatakiwa pia kushirikiana kwa pamoja katika kutatua matatizo ya watu wengine. Hivyo ndivyo imam alivyokuwa akifanya na hivyo ndivyo alivyokuwa akiwausia wafuasi wake.

Imepokelewa kuwa Waislamu wawili walihitilafiana baada ya kujiri mjadala baina yao. Sahaba mmoja wa imam aliyekuwa akifahamika kwa jina la Mufadh-dhal alipita eneo la tukio. Akiwa katika pitapita zake ndipo akafahamu kuwepo mjadala huo. Mufadh-Dhal akawachukua watu wale na kwenda nao nyumbani kwake na kuwambia:"Imam ameniamuru kwamba, popote pale nitakapoona tofauti kati ya Waislamu wawili, basi nirejeshe amani na udugu baina yao, na hata kama ikilazimu basi niwagawie mali za Imam. Hivyo chukueni hizi Dirham 400 ilimradi tu muweze kurejesha udugu wenu na muweke nguvu zenu pamoja."

Elimu ya Imam Sadiq AS

Imam Jafar Sadiq ambaye ni moja ya wajukuu watukufu wa Mtume Muhammad SAW, hakufanya kitendo chochote ambacho kinaweza kuhesabiwa kuwa moja ya sababu za kuibua farqa au kitendo ambacho hakitakuwa na maslahi kwa makundi au madhehebu mengine ya Kiislamu. Kunasibiana na Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW, elimu yake ya hali ya juu, akhlaqi njema na mambo mengine, ni miongoni mwa mambo yaliyokuwa yakiwavutia watu wengi na hivyo kumfanya mtukufu huyo kuwa kimbilio na marejeo ya watu na makundi mbalimbali wakati huo.

Kama vile ilivyopokelewa kwamba, katika msimu wa ibada ya hija Imam Sadiq AS alikuwa akikaa eneo la wazi kisha watu mbalimbali wakienda kando yake na kumuuliza maswali na yeye kuwajibu maswali yao.

Ahul Sunna wal-Jamaa na Imam Sadiq AS

Kukithiri watu waliokuwa wakienda kumtembelea mtukufu huyo, na mahusiano yake aliyokuwa nayo kwa matabaka ya watu tofauti, ni mamabo yaliyomtia wasi wasi mkubwa mtawala wa wakati huo, Mansur Dawaaniq. Abu Hanifa ambaye ni mwanachuoni maarufu na Imam wa madhehebu ya Hanafi ya Ahlusunna wal-Jamaa mbali na kumtaja Imam Sadiq AS kwamba alikuwa mtu mwenye elimu ya hali ya juu kati ya watu wote wa zama hizo anasimulia kisa cha kuvutia kuhusiana na mtukufu huyo kwa kusema:

"Siku moja Mansur aliniambia kwamba, watu wengi wamevutiwa sana na Imam Swadiq, hivyo andaa maswali magumu ili ufanye naye mjadala. Baada ya majlisi ya mjadala kuwadia, nilianza kumuuliza maswali yote huku Imam akiyajibu kwa kusema: Nyinyi mnaamini hivi, watu wa Madina wanaamini hivi na sisi tunaamini hivi. Katika baadhi ya mas'ala alikuwa akiafikiana nasi kama vile ambavyo alikuwa pia akiafikiana rai na watu wa Madina. Na sehemu nyingine alitofautiana na mirengo hiyo. Imam Sadiq AS alinijibu maswali yote 40 niliyokuwa nimeyaandaa ili kumshinda na kila swali alilijibu kwa mfumo huo. Je mtu anayefahamu tofauti za itikadi mbalimbali za watu si ndiye mtu mwenye elimu zaidi?"

Wanafunzi wa Imam Sadiq AS

Kati ya wanafunzi 4,000 wa mtukufu huyo, walikuwemo wafuasi wa madhehebu Ahlu Sunna Waljamaa, suala ambalo liliwafanya wasomi wa Ahlu Sunna kukubali marjaa ya kielimu ya Ahlu-Bayti wa Mtume SAW. Ni kwa ajili hiyo ndio maana katika mas'ala tofauti kama vile tafiri ya Qur'an na mengineyo, maulama hao wa Kisuni walikuwa wakienda kuuliza ufafanuzi wake kwa Imam Sadiq AS.

Aidha imepokewa kuwa, makadhi wa Kisuni walikua wakimwendea mjukuu huyo wa Mtume na kumuuliza kuhusiana na mas'ala ya kihistoria na kadhalika. Shakhsia kama Ma'adah bin Swadaqah ambaye alikuwa kadhi wa Kisuni, ni miongoni mwa makadhi maarufu waliofika kwa imam kuuliza masuala tofauti.

Aidha Ahlul-Bayt wa Mtume walikuwa nao kwa upande mwingine wakiwazuru watu hao na kuwatembelea sambamba na kutatua matatizo yao tofauti ya kielimu na kimada, na kufuta kabisa mwanya wa mahusiano kati ya Masuni na Mashia, na kujengeka mapenzi makubwa baina ya Waislamu wa madhehebu tofauti katika kipindi cha Imam Sadiq AS. Ni kwa ajili hiyo ndio maana Ahlul-Bayti wa Mtume SAW. wakahesabika katika jamii kuwa sawa na baba kwa watoto wake, katika juhudi zao za kuuepusha umma na hatari yoyote ya upotofu na bidaa.

Imam Abu Hanifa na Imam Malik wamsifu Imam Sadiq

Aidha miongoni wa wanafunzi wa Kisuni waliokuwa wakisoma kwa mtukufu huyo, ni pamoja na Abu Hanifa mwenyewe (Nuuman bin Thabit) na Malik bin Anas. Kuhusiana na Abu Hanifa amenukuliwa akikiri kwa kusema: "Mimi nilikuwa mwanafunzi halisi wa Jafar bin Muhammad." Anasema katika sehemu nyingine amesema kwamba: "Lau kama si miaka miwili niliyosoma kwa mtukufu huyo, basi ningeangamia."

Naye kwa upande wake Malik bin Anas ambaye ni Imam wa madhehebu ya Maliki anasimulia kumuhusu Imam Swadiq kwa kusema:"Katika kipindi ambacho nilikuwa nikisoma kwa Jafar bin Muhammad nilimuona na hali kuu tatu, aidha alikuwa akisali, au alikuwa amefunga saumu au alikuwa akisoma Qur'an na kamwe sikuwahi kumuona akiwa hayuko katika hali ya udhu. Hakuna mtu yeyote aliyemfikia Jafar bin Muhammad katika elimu na uchaji Mungu ..."

Kuuawa Shahidi

Pamoja na yote hayo na kutokana na chuki za maadui Imam Swadiq aliuawa shahidi katika siku kama ya leo. Baada ya kuuawa shahidi, mwili wa mtukufu huyo ulizikwa katika makaburi ya Baqii mjini Madina. Ulimwengu ukaomboleza kwa kuondokewa na mtukufu huyo. Sisi sote ni wa Allah na sote tutarejezwa Kwake.

Tunamalizia kwa baadhi ya miongozo ya Imam Swadiq AS aliponukuliwa akisema: Staha na haya ina vipengee kumi na vipengee tisa kati ya hivyo kumi vinapatikana kwa wanawake na kipengee kimoja kilichobakia kiko kwa wanaume.

captcha