IQNA

Kulaani tu hakutatatua matatizo ya Waislamu wa Rohingya

12:17 - September 06, 2017
Habari ID: 3471161
TEHRAN (IQNA)-Mwanazuoni wa Kiislamu nchini Lebanon amesema kunahitajika hatua za kivitendo kusitisha mauji ya umati ya Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar.

Katika mahojiano na IQNA, Sheikh Ahmad al-Qattan amesema Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu OIC inapaswa kuchukua hatua imara na za kivitendo kuwasaidia.

Amesema Waislamu wote wanapaswa kuchukua msimamo wa pamoja kuhusu masaibu yanayowasibu wenzao huko Myanmar. Sheikh al-Qattan ambaye ni mkuu wa Jumuiya ya Qawluna wal-Amal (Tunasema na Tunatenda) nchini Lebanon amesongeza kuwa kulaani tu hakutoshi kuwasaidia Waislamu wa Myanmar. Halikadhalika amelaani kimya cha jamii ya kimataifa kuhusu maafa ya Waislamu nchini Myanmar huku akitoa wito kwa watu wote duniani kuwasaidia Waislamu hao pasina kujali dini.

Taarifa zinasema zaidi ya Waislamu 3,000 wameuawa kwa umati tokea wimbi jipya la ukatili wa jeshi katika jimbo lenye Waislamu wengi la Rakhine nchini Myanmar.

Pamoja na kuwepo ushahidi wa mauaji ya kimbari ya Waislamu na hata baada ya kuzuiwa mashirika ya Umoja wa Mataifa kuingia katika jimbo la Waislamu la Rakhine nchini Myanmar, jamii ya kimataifa haijachukua hatua zozote za maana na imefumbia macho ukandamizaji huo wa Waislamu. Halikadhalika vyombo vya habari vya Magharibi pia kwa ujumla vimepuuza mauaji ya Waislamu nchini Myanmar huku baadhi wakidai kuwa eti waliouawa ni magaidi.

Katika miaka ya karibuni, Waislamu wengi wa kabila la Rohingya nchini Myamnar wameuawa au kulazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za jirani kutokana na mashambulio ya Mabuddha wenye misimamo ya kufurutu mpaka wanaoungwa mkono na serikali ya nchi hiyo.

3463856

captcha