IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Nchi za Kiislamu zichukue hatua za kivitendo kuwasaidia Waislamu Myanmar

17:30 - September 12, 2017
Habari ID: 3471169
TEHRAN (IQNA)-Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekosoa kimya na kutochukua hatua jumuiya za kimataifa na wanaojigamba kuwa watetezi wa haki za binadamu kuhusiana na matukio ya maafa yanayojiri Myanmar.
Aidha amesisitiza kuwa, njia ya utatuzi wa kadhia ya Waislamu wa Myanmar ni kuchukuliwa hatua za kivitendo na nchi za Kiislamu na kuishinikiza kisiasa na kiuchumi serikali isiyo na huruma ya Myanmar.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo asubuhi ya leo mjini Tehran wakati wa kuanza darsa ya Fiqhi ambapo sambamba na kutilia mkazo ulazima wa nchi za Kiislamu kuchukua hatua za kivitendo amesema: Tab'an madhumuni ya kuchukua hatua za kivitendo si kupeleka majeshi bali zinapaswa kuzidisha mashinikizo ya kisiasa, kiuchumi na kibiashara kwa serikali ya Myanmar na kupaza sauti zao dhidi ya jinai hizi katika jumuiya za kimataifa.

Ayatullah Khamenei amebainisha kuwa kuna udharura kwa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kuitisha mkutano wa kuzungumzia maafa ya Myanmar na kuongeza kwamba: Dunia ya leo ni dunia ya dhulma na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapaswa kudumisha sifa hii ya kujivunia iliyonayo ya kutangaza kinagaubaga na kwa ushujaa msimamo wake dhidi ya dhulma inayofanyika sehemu yoyote ile duniani, iwe ni katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni, Yemen, Bahrain au Myanmar.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza pia kwamba si sahihi kuyahafifisha maafa ya Myanmar kwa kuyataja kuwa ni mapigano ya kidini tu baina ya Waislamu na Mabudha na akaongezea kwa kusema: Bila ya shaka inawezekana katika kadhia hii taasubi za kidini nazo pia zikawa na taathira, lakini hii ni kadhia ya kisiasa kwa sababu mtendaji wake ni serikali ya Myanmar na katika nafasi ya juu kabisa ya serikali hiyo kuna mwanamke asiye na huruma ambaye ni mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobeli; na ukweli ni kwamba matukio yanayojiri ni sawa na kifo cha Tuzo ya Amani ya Nobeli.

Ayatullah Khamenei vilevile amemkosoa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa kutosheka na kutoa tamko la kulaani tu jinai za Myanmar na akaeleza kwamba: Wanaojigamba kuwa watetezi wa haki za binadamu ambao baadhi ya wakati huzusha zogo na makelele wakati inapotokea mhalifu mmoja akahukumiwa katika nchi fulani hawaonyeshi radiamali wala jibu lolote kwa mauaji na kufanywa wakimbizi makumi ya maelfu ya watu nchini Myanmar.

3640919


captcha