IQNA

Daktari Muislamu katika kampeni ya kuwa gavana wa kwanza Muislamu Marekani

17:13 - September 16, 2017
Habari ID: 3471177
TEHRAN (IQNA)-Daktari Abdul El-Sayed, mwenye umri wa miaka 32 kutoka mji wa Detroit jimboni Michigan, anaendeleza kampeni kali ya kutaka kuwa gavana kwa kwanza Mwislamu Marekani.

Daktari Abdul El-Sayed ambaye ni wa chama cha Democrats aanaendeleza kampeni kubwa na anazidi kupata umashuhuri mkubwa kiasi cha kufanikiwa kuchangisha dola milioni 1 za kampeni kwa muda mfupi sana. Yeye ni miongoni mwa Wademokrat wanne wanaowania kuteuliwa na chama hicho kukabiliana na moja kati ya Warepublican watatu ambao pia wanataka kupata tiketi ya chama hicho kugombea ugavana wa Michigan. Daktari Abdul El-Sayed anatazamiwa kuwezesha chama chake kuchukua tena udhibiti wa jimbo la Michigan ambalo kwa miaka minane sasa linadhibitiwa na Warepublican.

Jimbo la Michigan lina idadi kubwa zaidi ya watu wenye asili ya Kiarabu Marekani na wengi wanauliza iwapo wakati haujafika sasa kuwa na gavana Mwislamu.

Daktari El-Sayed aliteuliwa na Meya wa Michigan Mike Duggan kuwa Afisa Mkuu wa Afya na Mkuregenzi Mtendaji wa Idara ya Afya ya Detroit mwaka 2015 na hivyo kuwa kamshina mchanga zaidi wa afya katika mji mkubwa nchini Marekani. Wakati akitangaza uamuzi wake wa kugembea ugavana Daktari El-Sayed alisema: "Nagombea kwa sababu naamini nitakuwa gavana bora zaidi katika jimbo la Michigan-niwe au nisiwe Mwislamu. Imani yangu ni muhimu kwangu kama amabvyo ni muhimu kwa Wamarekani na Wamichigan."

Iwapo atacahguliwa, si tu kuwa Daktari El-Sayed atakuwa gavana wa kwanza Mwislamu Marekani bali pia atakuwa gavana mwenye umri wa chini zaidi Marekani tokea rais wa zamani Bill Clinton alipochaguliwa gavana wa Arkansas mwaka 1978.

Daktari huyo alihitimu Chuo Kikuu cha Tiba cha Michigan na kisha kupata Shahada ya Uzamili (MA) katika Chuo Kikuu cha Columbia kabla ya kupata Shahada ya Uzamifu katika uga wa afya ya jamii kutoka Chuo Kikuu cha Oxford.

Huenda El-Sayyed akapata matatizo katika kampeni zake kufuatia ongezeko kubwa la chuku dhidi ya Uislamu na Waislamu Marekani. Uchaguzi wa ugavana wa jimbo la Michigan umepangwa kufanyika Novemba 6. 2018.

3463919

captcha