IQNA

UAE yalaaniwa kwa kupendekeza serikali za Ulaya zidhibiti misikiti

21:41 - November 17, 2017
Habari ID: 3471267
TEHRAN (IQNA)-Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamelaani matamshi ya afisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ambaye amezitaka nchi za Ulaya ziwe na udhibiti katika misikiti ili kuzuia hujuma za “kigaidi”.
UAE yalaaniwa kwa kupendekeza serikali za Ulaya zidhibiti misikiti"Huwezi ukawa na msikiti uliowazi na kumruhusu kila mtu aingie kuswali na kuhubiri,” alisema Sheikh Nahyan bin Mubarak al Nahyan, Waziri wa Stahamala wa UAE Jumanne wiki hii katika mahojiano na Shirika la Habari la Ujerumani, DPA.

Sheikh Nahyan amenukuliwa akisema, Ujerumani inapaswa kuchukua hatua kama zilizochukuliwa na serikali za Ufaransa, Uingereza na Ubelgiji za kudhibiti kikamilifu misikiti.

Kufuatia kauli hiyo, Jumuiya ya Kiarabu ya Haki za Binadamu nchini Uingereza (AOHR UK) imetoa taarifa na kulaani matamshi ya waziri huyo wa UAE na kusema huo ni uchochezi dhidi ya Waislamu wa Ulaya.

"Iwapo mtu anaswali katika msikiti kisha atekeleze kitendo cha uhalifu, hilo halimaanishi wale wote wanaoswali katika msikiti huo wanaunga mkono kitendo hicho cha uhalifu wala haimaanishi msikiti unaunga mkono uhalifu huo, " imesema taarifa ya AOHR UK.

Taarifa hiyo imesema hivi sasa misikiti barani Ulaya tayari inaendeshwa kwa mujibu wa sheria kali zilizowekwa.

Aidha AOHR UK imetoa wito kwa nchi za Ulaya kutotekeleza pendekezo la Sheikh Nahyan kwani litaigeuza misikiti Ulaya kuwa vituo vya ujasusi.

Pendekezo hilo la UAE halikuwashangaza wengi kwani utawala huo wa kifalme unadhibiti kikamilifu misikiti katika nchi hiyo.

3464438

captcha