IQNA

Inna Lillah wa Inna Ilayhi Rajioun

Qarii na mwanazuoni maarufu wa Qur'ani Libya, Sheikh Qashqash aaga dunia

19:11 - September 15, 2018
Habari ID: 3471671
TEHRAN (IQNA)-Qarii na mwanazuoni mtajika wa Qur'ani Tukufu nchini Libya na katika ulimwengu wa Kiislamu Sheikh Mustafa Qashqash amefariki dunia na kuzikwa Ijumaa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli.

Vyombo vya habari vya Libya vimearifu kuwa marhum Sheikh Mustafa Qashqash alizikwa Ijumaa Septemba 14 baada ya sala ya Ijumaa. Mwanazuoni huyo ambaye pia alikuwa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Uchapishaji Qur'ani Tukufu nchini Libya alizikwa katika Makaburi ya Ould Moussa mjini Tripoli.

Sheikh Mustafa Qashqash ambaye kadhalika alikuwa Hafidh wa Qur'ani Tukufu aliaga dunia mapema Ijumaa akiwa na umri wa miaka 83 na maziko yake yalihudhuriwa na idadi kubwa ya jamaa, marafiki, wanafunzi wake na waumini kwa jumla.

Mwanazuoni huyo wa Qur'ani alizaliwa mwaka 1935 Miladia na alifanikiwa kuhifadhi Qur'ani Tukufu utotoni na kisha akaelekea katika Chuo Kikuu cha Zeituniya nchini Tunisia kuendeleza masomo yake. Alianza kufunza Qur'ani Tukufu tokea mwaka 1962 hadi mwaka 1986 na kuanzia mwaka 1972 hadi 1998 alikuwa pia mmoja wa wanachama wa kamati ya tafsiri ya Qur'ani Tukufu nchini Libya.

Mbali na kushiriki katika mashindano ya kitaifa na ya kimataifa ya Qur'ani Tukufu, halikadhalika alikuwa jajai ya mashindano kadhaa ya Qur'ani ya kimataifa yakiwemo ya Dubai, Saudia, Tunisia, Syria, Pakistan na Uturuki.

Qarii na mwanazuoni maarufu wa Qur'ani Libya, Sheikh Qashqash aaga dunia

Marhum Sheikh Mustafa Qashqash na wanafunzi wake

/3746836

captcha