IQNA

Watoto Waislamu China watenganishwa na wazazi wao, ukandamizaji wazidi

15:02 - September 21, 2018
Habari ID: 3471682
TEHRAN (IQNA)- Utawala wa China unawatenganisha watoto Waislamu na wazazi wao ambao wanashikiliwa katika gereza au kambi maalumu za mafunzo ya Kikomunisti.

Hayo yanajiri huku serikali ya Beijing ikizidisha ukandamizaji wake wa Waislamu wa jamii ya Uighur nchini humo.

Katika mfano wa hivi karibuni ni Bi. Meripet ambaye anasema akiwa na mume wake walisafiri kutoka China kuenda Uturuki kumjulia hali baba yake mgonjwa. Lakini baada ya serikali kuanza kuwakamata kiholelea Waislamu wa jamii wa Uighur kwa madai mbali mbali, safari yao ya  Uturuki ilitajwa kuwa ni ya kichochezi na hivyo hawajaweza kurudi nyumbani kwa kuhofia kukamatwa. Watoto wake wanne walichukuliwa na mama mkwe wake ambaye naye alikamatwa katika oparesheni dhidi ya Waislamu.

Baada ya tukio hilo watoto hao walio na umri wa kati ya miaka 3-8 walichukuliwa na serikali ya eneo la Xinjiang na kuwekwa katika kituo cha mayatima ambacho Bi. Meripet amekitaja kuwa ni sawa na gereza. Familia ya Meripet ni mfano wa idadi kubwa ya familia za Waisalmu ambazo zimeswekwa gerezani na serikali ya Rais Xi Jinping wa China. Hayo yanajiri wakato amabo hivi karibuni Wataalamu wa haki za binadamu katika Umoja wa Mataifa wametoa wito kwa China kuwaachilia huru mara moja Waislamu wanaoshikiliwa katika kambi za kuwafunza Ukomunisti na kwa kisingizio cha kukabiliana na ugaidi.

Taarifa zinasema wakuu wa utawala wa China wanawashikilia kwa nguvu Waislamu karibu milioni 1 wa jamii ya Uighur katika kambi zenye msongamano mkubwa ambapo wanafunzwa kwa lazima itikadi za Kikomunisti mkoani Xinjiang.

Waliowahi kuwa katika kambi hizo wanaema wanaoshikiliwa wanalazimishwa kula nyama ya nguruwe na kunywa pombe kinyume cha mafundisho ya Kiislamu.

Mkoa wa Xinjiang una wakazi Waisalmu zaidi ya milioni 10 kutoka kabila la Uighur na katika miaka ya hivi karibuni eneo hilo limeshuhudia makabiliano makali baina ya wanajeshi na Waislamu.

3748657

captcha