IQNA

Wanigeria waandamana Abuja wakitaka Sheikh Zakzaky aachiliwe huru

19:55 - July 08, 2020
Habari ID: 3472942
TEHRAN (TEHRAN) - Wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria wameandamana katika mji mkuu wa nchi hiyo Abuja wakitangaza uungaji mkono wao kwa Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa harakati hiyo ambaye anaendelea kushikiliwa kizuizini licha ya hali yake mbaya ya afya.

Waandamanaji hao wakiwa wamebeba mabango na maberamu walisikika wakipiga nara za kulaani kuendelea kushikiliwa Sheikh Ibrahim Zakzaky pamoja na mkewe Malama Zeenat huku wakitaka wawili hao waachiwe huru haraka iwezekanavyo.

Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imesema katika taarifa yake ya jana Jumanne kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, Sheikh Zakzaky ambaye anazuiliwa kinyume cha sheria anapaswa kuachiwa huru mara pasina masharti yoyote. Wanachama wa harakati hiyo wamesema wataendelea na maandamano yao kila siku mjini Abuja hadi pale kilio chao kitakaposikika.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, tarehe 2 Disemba 2016 Mahakama Kuu ya Nigeria ilitoa hukumu kwamba kutiwa mbaroni Sheikh Zakzaky na mkewe ni kinyume cha sheria na kunakinzana na katiba ya nchi hiyo, hivyo wanapaswa kuachiwa huru.

Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe Malama Zeenat walitiwa nguvuni tarehe 13 Desemba 2015 wakati wanajeshi wa Nigeria walipovamia Hussainia ya Baqiyatullah na nyumba ya mwanazuoni huyo katika mji wa Zaria. Waislamu wasiopungua 1,000, wakiwemo watoto watatu wa kiume wa Sheikh Zakzaky, waliuawa shahidi katika shambulio hilo.

Hatua kandamizi na za kikatili za polisi na jeshi la Nigeria dhidi ya wafuasi wa Sheikh Zakzaky zingali zinaendelea na hadi sasa idadi kubwa ya wafuasi wa kiongozi huyo wa kidini wamewekwa kizuizini au wameuawa shahidi.

3909293

captcha