IQNA

Imam Ridha AS, alim mwenye fadhila na ubora wa kimaanawi

20:32 - June 21, 2021
Habari ID: 3474029
TEHRAN (IQNA)- Tuko katika kumbukumbu ya kuzaliwa Imam Ridha AS, mmoja kati ya Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad SAW.

Miaka 1294 iliyopita, sawa na tarehe 11 Dhulqaada mwaka 148 Hijria, alizaliwa Imam Ali bin Mussa Ridha AS, mmoja kati ya Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad SAW katika mji wa Madina.

Imam Ridha alichukua jukumu la kuwaongoza Waislamu mara baada ya kufariki dunia baba yake, Imam Mussa al-Kadhim AS, mnamo mwaka 183 Hijria. Shakhsia huyo alikuwa mbora zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu wakati wa zama zake. Kwa minajili hiyo, Ma'amun, Khalifa wa Kiabbasi alijaribu kumpatia wadhifa Imam Ridha AS kwa shabaha ya kuimarisha nafasi yake na wakati huo huo kumdhibiti mjukuu huyo wa Mtume. Imam Ridha AS alikubali pendekezo hilo kwa kulazimishwa na kwa mashinikizo ya utawala wa Ma'amun. Mtukufu huyo aliwaeleza Waislamu wote, wakiwemo watu wa eneo la Khorasan, ukweli wa mambo ulivyo, na kuwaathiri mno wananchi kuhusiana na uhakika wa Ahlul-Bait wa Mtume AS.

Milango ya Hekima

Imamu huyo mkarimu ambaye alikuwa mbeba bendera ya Wilaya, katika kipindi chote cha maisha yake yaliyojaa baraka aliufungulia Umma milango ya hekima na maarifa na hivyo akawa kigezo cha ucha Mungu na ubora kwa lengo la kufikia saada. Tunachukua fursa hii kutoa salamu zetu za rambi rambi kwa mnasaba wa kukumbuka kuuawa shahidi Imamu huyu mkubwa na kuwakaribisha kusikiliza machache tuliyowaandalia kumhusu.

Imam Ridha AS aliishi sehemu ya maisha yake katika zama za utawala wa Ma'amun, khalifa wa silisili ya Bani Abbas. Ma'amun alikuwa mtu mwenye ujanja wa kisiasa na hila na alijiarifisha kama mtu apendaye elimu.

Mara kwa mara alikuwa akiandaa vikao vya kielimu vilivyohudhuriwa na Imam Ridha AS na wasomi wengine wa kidini na kimadhehebu ili wafanye midahalo.

Lengo la Ma’amun lilikuwa ni kutia dosari shakhsia ya kielimu ya Imam. Lakini kinyume na alivyotarajia Ma’amun, vikao hivyo vilipelekea shakhsia iliyojaa fadhila na elimu ya Imam Ridha AS kubainika wazi kwa wote. Hii ni kwa sababu Imam Ridha AS alijibu kikamilifu maswali yote aliyoulizwa katika nyanja mbali mbali za kielimu. Ujuzi mkubwa na elimu ya hali ya juu ya Imam ni jambo ambalo lilipelekea Ma’amun kukiri kuwa: “Hakuna mtu mwenye ujuzi mkubwa duniani kumliko Hadhrat Ridha.”

Sifa za Imam

Imam Ridha AS alibainisha moja ya sifa muhimu za Imamu kwa kusema Imamu anatakiwa kuwa na elimu na uono wa mbali au hekima. Imam Ridha AS amenukuliwa akisema: “Elimu na ujuzi wa Imam daima huwa unastawi, huwa ni mpole, mwenye kufahamu kikamilifu masuala ya kisiasa na huwa ni mwenye kustahiki uongozi. Imam ni mlinzi wa dini ya Mwenyezi Mungu na kuwalingania watu kwa hekima, mawaidha, uzuri na hoja za wazi ili waelekee katika njia ya Mwenyezi Mungu.”

 

Kuhuisha Uislamu

Imam Ridha AS kwa kuzingatia kikamilifu matukio ya kielimu na kisiasa ya zama, alitekeleza ipasavyo risala yake kwa lengo la kuhuisha Uislamu wa kweli na kuwaongoza wanaadamu katika njia ya haki. Kwa kutumia fikra zake za Uislamu halisi, mtukufu huyo aliwaondoa wanaadamu kutoka njia potofu na kuwaongoza katika njia iliyonyooka. Kwa hakika Imam Ridha AS alikuwa mfano wa daraja la mawasiliano baina ya waja na Allah SWT na hivyo kuwafanya waweze kufahamu kwa kina mafundisho yenye thamani ya Kiislamu. Daima mtukufu huyo alikuwa akitoa wito kwa watu kutafakari na kuwa na tadbiri katika dini kwa kusema: “Ibada si kufunga na kuswali kwa wingi bali ibada (ya kweli) ni kutafakari sana kumhusu Allah SWT.”

Miongoni mwa Maimamu waliotakasika, Imam Ridha AS alipata lakabu ya “Alim Aali Mohammad” yaani  ‘Msomi wa Kizazi cha Mohammad.'

Hali bora zaidi kwa mwanaadamu ni kunyenyekea na kuwa na khushuu mbele ya Allah SWT. Kuhusu hili Imam Ridha AS alisema: “Hali ya kuwa karibu zaidi mja na Allah SWT ni katika hali ya kusujudu na hili linaenda sambamba na ile kauli ya Allah Tabaraka wa Ta’ala aliposema:  ‘Sujudu ili ukaribie.”

 

Sifa za Imani

Ali bin Musa Ridha AS katika hadithi anasema hivi: “Hakuna mja anayefikia uhakika wa imani isipokuwa awe na sifa tatu: Maarifa na ufahamu katika dini, msimamo wa wastani katika maisha na subira katika misiba.”

Kimsingi ni kuwa mwanaadamu hufikia imani kamili anapokuwa na maarifa kamili, khushuu na kutekeleza faradhi za kidini kwa uono wa mbali. Katika utumizi wa fedha katika maisha vile vile hapaswi kuwa na misimamo ya kufurutu mipaka na katika matatizo ya maisha Mwislamu anapaswa kuwa mstahamilivu na kukubali takdiri ya Mwenyezi Mungu.

Katika zama za khalifa wa Bani Abbas, Ma’amun baadhi ya wakati alikuwa akiwaita wasomi wa taaluma ya tiba kutoka maeneo mbali mbali kwa lengo la kufanya midahalo ya kisayansi ili kwa njia hiyo aweze kupata itibari.

Sayansi ya Tiba

 

Katika moja ya vikao hivyo vya kisayansi alihudhuria Imam Ridha AS na Ma’amun ambapo kundi la matabibu na wanafalsafa maarufu wa Nishabur walihudhuria. Walitoa hotuba nyingi kuhusu masuala ya kitiba. Imam Ridha AS alikaa kimya na kutosema chochote. Ma’amun alumwambia hivi Imam Ridha AS: "Ya Abal Hassan! Una nini cha kusema kuhusu maudhui hizi?"

Imam alisema: “Nina maoni ambayo usahihi wake nimeupata kupitia tajriba ya muda mrefu. Zaidi ya hayo nina elimu ambayo waliotangulia waliniachia na kuna mambo ambayo kila mwanaadamu anapaswa kuyajua. Nitakusanya nadharia hizi na tajriba pamoja na yote yanayohitajika katika uga huu.”

Imam alitayarisha risala yake na kumkabidhi Ma’amun. Ili kuonyesha umuhimu wa risala hiyo, Ma’amun aliamuru iandikwe kwa wino wa dhahabu na ihifadhiwe katika hazina ya serikali. Ni kwa sababu hii ndio ikapewa jinal la “Risalatul Dhahabiyya.” Hivi ndivyo mjumuiko huu wa maelezo ya kitiba ya Imam Ridha AS kuhusu afya ya mwili ulikusanywa katika risala hiyo iliyopewa jina la Dhahabiyya. Katika risala hii Imam amesherehesha faida za vyakula mbali mbali, mbinu za kitiba na kiafya pamoja na namna ya kukabiliana na maradhi ya kiroho na kinafasi.

Risala hii imejaa siri nyingi. Katika risala hii Imam ameandika hivi: “Mwenyezi Mungu hajaufanya mwili uwe na ugonjwa isipokuwa ameujaalia uwe na dawa ya kutibu…”

Katika sehemu ya kitabu hicho chenye thamani ambacho pia ni maarufu kama ‘Tibb Ar Ridha’, Imam Ridha AS amesema: “Iwapo watu wataridhika kula chakula kichache, miili yao itakuwa na mlingano.”

Risala hii ya tiba iliyojaa balagha ni kati ya vitabu vyenye thamani kubwa vya Kiislamu katika uga wa tiba. Kitabu hicho kimebainisha maudhui mbali mbali za kitiba kama vile biolojia, fiziolojia, kemia, lishe n.k. Kitabu hiki kinamuongoza mwanaadamu katika maisha bora yenye afya ambayo ni neema kubwa ya Allah SWT.

Khalifa wa Kiabbasi

Naam, Imam Ridha AS alikuwa shakhsia adhimu na alim mwenye fadhila. Alikuwa na ubora wote wa kimaanawi na kimaadili. Alichukua jukumu la Uimamu na kuuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 35. Mtukufu huyo alikuwa kipenzi cha Umma. Lakini Ma’amun, Khalifa wa Kiabbasi hakuweza kustahamili mahaba makubwa ya watu kwa Imamu Ridha AS pamoja na karama zake nyingi. Katika upande mwingine hakuweza kuzuia ushawishi wa kimaanawi wa Imam Ridha na hivyo akawa anamtazama kama kizingiti katika malengo yake machafu. Kwa hivyo Ma’amun alitumia kila njama kuhakikisha anamuondoa Imam katika njia yake. Alitekeleza njama yake hiyo chafu katika siku ya mwisho ya mwezi wa Safar mwaka 203 Hijria na hatimaye kumuua shahidhi Imam Ridha AS.

Haram Takatifu ya Imam Ridha AS iko katika mji wa Mashhad, kaskazini mashariki mwa Iran. Kila mwaka wakati wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Imamu huyo mtoharifu, wafanyaziara kutoka Iran na maeneo mengine duniani humiminika Mashhhad kwa lengo la kuadhimisha uzawa huu uliojaa baraka.

captcha