IQNA

Qur'ani Tukufu iliyotarjumiwa kwa lugha ya Kalenjin yazinduliwa Kenya

16:38 - November 14, 2021
Habari ID: 3474557
TEHRAN (IQNA)- Lugha ya Kalenjin nchini Kenya inakadiriwa kuwa na wazungumzaji milioni 6.3 na sasa jamii hiyo kubwa kwa mara ya kwanza imepata Qur'ani Tukufu iliyotarjumiwa kwa lugha yao.

Jamii ya Kalenjin ina makabila mengine madogo 11 ambayo ni Ogiek, Nandi, Keiyo, Sabaot, Lembus, Tugen, Terik, Nandi, Marakwet, Pokot na Kipsigis.

Waislamu katika jamii ya Kalenjin kwa muda mrefu wamekuwa na tatizo la kuifahamu Qur'ani Tukufu kwa sababu wengi hawafahamu Kiarabu, Kiingereza au Kiswahili. Lakini sasa tatizo hilo limeweza kutatuliwa kwani tarjuma ya Qur'ani Tukufu kwa lugha ya Kalenjin, Kuran ne Toroor, imezinduliwa.

"Tulikuwa na changamoto kubwa. Watu wengi katika jamii yetu wanaipenda sana lugha yao. Kwa kuzingatia kuwa wengi hawafahamu Kiarabu, Kiswahili au Kiingereza sana, tumekuwa tukitegemea wahubiri na waalimu wa Madrassah kufasiri Qur'ani wanapozungunza," amesema Bilal ibn Kipkorir wa jamii ya Kalenjin katika mazungumzo na waandishi habari.

Kipkorir ambaye kawaida huswali katika Masjid Fahilah Eldoret magharibi mwa Kenya amewashukuru wale wote walioshiriki katika mradi wa kuhakikisha kuwa Qur'ani Tukufu inapatikana kwa lugha ya Kikalenjin.

Hii ni mara ya kwanza kabisa kwa Qur'ani Tukufu kutarjumiwa kwa lugha ya Kalenjin. Kazi hiyo nzito ya tarjuma imefanikishwa na Sheikh Suleiman Kiptoo Sugoi ambayo anafahamu kikamilifu lugha ya Kalenjin na lahaja zake mbali mbali na pia ni mweledi wa lugha za Kiarabu na Kiingereza. Alishirikiana na wanazuoni wa Kiislamu nchini Kenya katika kuhakikisha kuwa kazi hiyo inafanyika kwa ustadi wa hali ya juu. Anasema lengo la mradi huo ni kuhakikisha kuwa jamii ya Kalenjin ambayo pia inapatikana nchini Uganda inapata uelewa sahihi wa Qur'ani Tukufu na Uislamu.

"Tumezindua Qur'ani Tukufu kwa lugha ya Kalenjin na mradi huu umechukua miaka 10 kukamilika. Lengo langu ni kuhakikisha kuwa jamii ya Kalenjin inaifahamu Qur'ani na kutekeleza amfundisho yake," amewaambia waandishi habari wakati wa uzinduzi mwezi Oktoba.

Gavana wa Jimbo la Uashin Gishu , lenye idadi kubwa ya Wakalenjin, Jackson Mandago amepongeza hatua hiyo ya kufasiriwa Qur'ani Tukufu kwa lugha ya Kalenjin na kusema hatua hiyo itawawezesha wengi kuufahamu Uislamu. "Kizingiti kikubwa katika kuufahamu Uislamu ni lugha. Tarjuma hii itatuwezesha kuifahamu dini ya wenzetu Waislamu na mradi huu utaleta maelewano katika jamii," amesema. Ameongeza kuwa, "nampongeza Sheikh Sugoi kwa kazi hii tukufu. Mimi kama gavana wake nina fakhari kubwa."

Kwa upande wake, Hassan Ole Naado, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Kenya (SUPKEM) amempongeza Sheikh Sugoi na kusema Qur'ani Tukufu ina mafunzo yote ya maisha katika sekta kama vile utamaduni, sheria,uongozi, amani na maelewano na kuongeza kuwa, "hii ndio sababu amani ni msingi katika mfumo wa Kiislamu wa maisha."

3476479

captcha