IQNA

Uislamu na Mazingira

Misri yazindua kitabu kuhusu Uislamu unavyosisitiza kulinda mazingira

18:29 - November 06, 2022
Habari ID: 3476043
TEHRAN (IQNA) - Wizara ya Wakfu ya Misri siku ya Jumamosi ilizindua kitabu kuhusu uhusiano kati ya mazingira na Uislamu.

Kitabu hicho kimezinduliwa wakati mazungumzo muhimu ya kimataifa mabadiliko ya tabianchi COP27, yanaanza leo huko Sharm-el Sheikh nchini Misri,

Kitabu hicho kilichopewa anuani ya  "Kulinda Mazingira Kati, Wajibu wa Kisheria na Binadamu," kinaangazia  namna Uislamu unavosisitiza kuhusu  mazingira ya dunia na kuyatunza kwani ni  mali ya umma.

Waziri wa Wakfu, Sheikh Mohamed Mukhtar Gomaa na wanazuoni kadhaa walichangia katika kitabu hicho, ambacho kinaeleza jinsi Shariah ya Kiislamu inavyotoa mazingatio maalumu katika kulinda mazingira kwa sababu  jambo lolote linalosaidia kufikia maslahi ya nchi na watu wake ndio msingi wa Uislamu

 "Dini yetu inahusika na suala la mazingira na haja ya kuyalinda kama mali ya umma," Sheikh Gomaa alisema katika utangulizi wake wa kitabu hicho.

Aliongeza kuwa hatari zitokanazo na mazingira kuharibiwa zimeongezeka na kuongezeka kwa njia ambayo inatishia ubinadamu wote.

Miongoni mwa tafiti zilizomo ndani ya kitabu hicho ni utafiti wa Mohammed Al-Jabali, mkuu wa Idara ya Sharia ya Chuo Kikuu cha Al-Azhar, ambapo alisema: “Uislamu unatilia maanani sana utunzaji wa mazingira na sayari ya dunia  na umeweka kanuni zinazolenga kufanikisha mlingano wa ikolojia na uthabiti."

Aliongeza: “Maandiko ya kisheria yanaonya dhidi ya kudhuru mambo ya mazingira. Walichokubaliana wanachuoni ni kuhifadhi vitu muhimu vya maisha, kama vile dini, nafsi, watoto, akili, pesa na nchi.”

Katika utafiti tofauti kuhusu upandaji miti, Ahmed Abbas, mkurugenzi mkuu wa Shirika la Masuala ya Mazingira la Misri, alisema: "Wito wa kupanda miti katika mabustani, na hata paa za shule, vyuo vikuu na taasisi za serikali ni jambo linalostahili kuzingatiwa kwa sababu linafanikisha malengo ya mazingira, afya, kilimo, kijamii, maendeleo na kiuchumi.”

Mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa mkataba wa Kimataifa wa tabianchi COP27 mwaka huu unafanyika huko Sharm el-Sheikh,nchini Misri kuanzaia Novemba 6-16. Mkutano huo unafanyika wakati ambao takwimu za wanasayansi zinasisitiza kwamba ulimwengu haufanyi vya kutosha kukabiliana na utoaji wa hewa ya kaboni na kulinda mustakabali wa sayari yetu.

Mikutano wa nchi wanachama wa Mkataba wa Kimataifa wa tabianchi au kwa kifupi COPs ndio mikutano mikubwa na muhimu zaidi ya kila mwaka inayohusiana na tabianchi kwenye sayari.

3481143

captcha