IQNA

Jinai za Israel

Jeshi katili la Israel lampiga risasi na kumuua shahidi binti wa Mpalestina

20:33 - November 14, 2022
Habari ID: 3476089
TEHRAN (IQNA)- Wanajeshi makatili wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamemuua shahidi msichana wa Kipalestina aliyekuwa na umri wa miaka 19 katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Vyombo vya habari vya Palestina vimeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, binti huyo aliyetambuliwa kwa jina la Sana Al-Tal, ameuawa shahidi kwa kumiminiwa risasi na askari wa utawala haramu akiwa ndani ya gari lake katika mji wa Beytuna, magharibi mwa Ramallah katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Shirika la habari la al-Shahab limeandika kuhusu tukio hilo katika ukurasa wake wa Twitter na kueleza kuwa: Asubuhi hii, vikosi vya Israel vimelimiminia risasi gari moja katika mji wa Beytuna, ambapo mwanamke mmoja ameuawa shahidi, huku watu wengine kadhaa waliokuwa kwenye gari hilo wakikamatwa.

Wizara ya Afya ya Palestina imeripoti kuwa, binti huyo kwa jina la Sana Al-Tal ameuawa shahidi kwa kupigwa risasi kichwani na wanajeshi wa utawala ghasibu wa Israel waliouvamia mji wa Beytuna alfajiri ya leo. Mwanaume mmoja wa Kipalestina amejeruhiwa vibaya kwenye shambulio hilo.

Katika miezi ya hivi karibuni, askari makatili wa utawala wa Kizayuni wameshadidisha ukatili na jinai zao dhidi ya Wapalestina hususan katika miji ya Jenin na Nablus eneo la Ukingo wa Magharibi linalokaliwa kwa mabavu.

Ripoti iliyotolewa mapema mwezi huu wa Novemba na Wizara ya Afya ya Palestina inasema kuwa, Wapalestina zaidi ya 185 wameuawa shahidi na jeshi katili la Israel huko Ukingo wa Magharibi na katika Ukanda wa Gaza tokea mwanzoni mwa mwaka huu 2022.

 

3481251

captcha