IQNA

Tafsiri za Qur'ani Tukufu na Wafasiri/ 9

Makhzan al-Irfan; Tafsiri pekee kamili ya Qur'ani iliyoandikwa na mwanamke

13:04 - November 28, 2022
Habari ID: 3476160
TEHRAN (IQNA) – Mwandishi wa Tafsiri ya Qur'ani Tukufu ya Makhzan al-Irfan fi Tafsir al-Qur'an alikuwa ni mwanamke ambaye alifikia kiwango cha juu kabisa katika elimu ya Fiqh na alikuwamwanamke wa kwanza kuandika tafsiri nzima ya Qur'ani Tukufu.

Taarifa za kihistoria zinaonyesha kuwa vikao vya tafsiri ya Qur'ani vimekuwa vikifanyika katika ardhi za Kiislamu tangu karne za kwanza baada ya kuja kwa Uislamu. Lakini tunapopitia orodha ya wafasiri wa Qur'ani walioandikwa katika kipindi cha karne 14 zilizopita, tunafikia natija kwamba mwanamke pekee ambaye ameandika tafsiri ya Qur'ani Tukufu ni Banu-ye Mujtahidah Seyyedeh Nosrat Begum Amin al-Tujjar Isfahani, anayejulikana kama Banu Amin.

Aliandika Makhzan al-Irfan fi Tafsir al-Quran kwa Kiajemi au Kifarsi katika juzuu 15.

Kuhusu mwandishi

Banu Amin (1890-1982) alikuwa Mujtahid (alikuwa amefikia kiwango cha Ijtihad ambacho ni kiwango cha juu kabisa cha kielimu katika Fiqh). Hadhi yake ya kielimu ilikuwa ya juu sana hivi kwamba wanachuoni wakubwa kama vile Ayatullah Seyed Shahbeddin Mar’ashi Najafi na Allamah Amini walipata ruhusa kutoka kwake kusimulia Hadith.

Kufunza wanazuoni wengi, kuanzisha Hauza (seminari) ya Kiislamu ya wanawake katika mji aliozaliwa wa Isfahan, Iran ya kati, kuanzisha shule ya upili ya wasichana na kuandika idadi kubwa ya vitabu katika nyanja tofauti zilikuwa miongoni mwa huduma zake kwa Uislamu na Waislamu.

Vipengele vya Makhzan al-Irfan

Makhzan al-Irfan fi Tafsir al-Qur'an inachukuliwa kuwa miongoni mwa tafsiri za kina za Qur'ani Tukufu. Tafsiri hii inatoa maelezo ya aya kwa mtindo wa masimulizi na uchanganuzi. Njia yake kuu ni ya kiakhlaqi ya Kiirfani.

Ufafanuzi unaanza na dibaji ambayo mwandishi anataja msukumo wake wa kuandika tafsiri, fadhila ya Qur'ani Tukufu, Tafsir Bil Ray (aina ya Tafsir ya Quran ambayo msingi wake ni hoja na juu ya kile kinachoitwa 'Ijtihad' badala ya kuzingatia upokezaji wa elimu), na masuala mengine yanayohusiana na sayansi ya Quran.

Katika tafsiri yake, kwanza anataja aya kadhaa kisha anaanza kufafanua ujumbe wa aya hizo kwa lugha rahisi na sahali kueleweka. Mwandishi pia wakati mwingine ananukuu maneno kutoka kwa Mulla Sadra na wanafalsafa na wanairfani wengine.

Ama kuhusu madhumuni yake ya kuanza kazi hiyo, anaandika kwamba kwa muda alikuwa akifikiria mara kwa mara juu ya kuandika maelezo mafupi ya Qur'ani yanayonufaika na maneno ya Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (SAW) yaani Ahl-ul-Bayt (AS) na kutumia maandishi ya wafasiri waliotangulia na hatimaye alianza kwa kuandika tafsiri ya neno kwa neno ya na kutoa maelezo kuhusu baadhi ya Ayat al-Muhkamat (aya zilizo wazi na zisizo na utata).

 

Kutawala mtazamo wa kiirfani katika Makhzan al-Irfan

Mfasiri katika Makhzan al-Irfan fi Tafsir al-Quran anajaribu kufuatilia kuelimisha Nafs (nafsi) ya mwanadamu na kuipeleka mbali na mambo ya kidunia na kuileta karibu na Mwenyezi Mungu.

Banu Amin katika kazi hii amenufaika na wafasiri wa Qur'ani wa Shia na Sunni na ameyataja maoni yao. Miongoni mwa tafsiri za Quran ambazo amenufaika nazo ni pamoja na Tafsir ya Mulla Sadra, Majma al-Bayan, Tafsiri ya Qomi, Rawd al-Jinan wa Ruh al-Janan (pia inajulikana kama Tafsir Abu al- Futuh), Kashf al-Asrar, Al- Mizan, Al-Burhan, Tafsir al-Baydawi, na Al-Durr Al-Manthur Fi Tafsir Bil-Ma'thur cha al-Suyuti.

Aidha pia ametumia tafsiri za Maswahabah na Tabi’in kama vile Ibn Abbas, Ibn Mas’ud na Ikrima.

captcha