IQNA

Rais wa Iran

Siku ya Mwanachuo Iran ni nembo ya kumtambua adui

23:10 - December 07, 2022
Habari ID: 3476214
TEHRAN (IQNA)-Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameitaja Siku ya Mwanachuo kuwa ni nembo ya kumtambua adui, kukabiliana naye, kuwa makini na kuwajibika wanafunzi wa vyuo vikuu.

Jumatano ya leo inasadifiana na tarehe 16 Azar kwa kalenda ya Iran ya Hijria Shamsia na ni Siku ya Mwanachuo katika kalenda ya matukio ya Jamhuri ya Kiislamu.

Tarehe 16 Azar 1332 Hijria Shamsia iliyosadifiana na tarehe 7 Disemba 1953 wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Iran walifanya maandamano mbele ya Chuo Kikuu cha Tehran kulaani na kulalamikia ziara ya Richard Nixon, makamu wa rais wa wakati huo wa Marekani na uingiliaji wa Washington katika masuala ya ndani ya Iran. 

Maandamano hayo ya wanachuo yalikandamizwa na utawala kibaraka wa Pahlavi. Wanajeshi wa utawala huo wa kidikteta wa Shah waliua wanachuo watatu na kujeruhi mamia ya wengine kwenye maandamano ya siku hiyo. 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Ebrahim Raisi amesema katika hafla iliyofanyika kwa mnasaba wa tarehe 16 Azar katika Chuo Kikuu cha Tehran kuwa siku hii ni siku ya matumaini kwa nchi hii na kusisitiza kuwa, tarehe 16 Azar ni nembo na kielelezo cha fikra, ustawi na maendeleo, na kuelewa hali na alama za nyakati kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza kuwa chuo kikuu ni kituo cha fikra na ushauri na kuongeza kuwa, wanafunzi wanapaswa kuisaidia serikali kutatua matatizo.

Raisi amesisitiza kuwa wanafunzi wa vyuo vikuu hufuatilia masuala ya jamii zaidi na kwa njia bora zaidi, na kwamba anatambua suala la mawasiliano na wanafunzi wa vyuo vikuu kama fahari na fursa nzuri ya kufaidika na maoni ya wasomi.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria kuwa, hii leo chuo kikuu kimetoa dharuba na pigo kwa adui anayetaka kuzuia masoma na kujifunza sayansi na maendeleo ya kielimu, lakini wanafunzi na wahadhiri wa wamesambaratishai njama za adui.

Raisi amesisitiza kuwa, malalamiko yanapaswa kusikilizwa na kuongeza kuwa: Malalamiko ni tofauti kabisa na machafuko; kwa sababu malalamiko huwa sababu ya marekebisho na ukamilifu, na machafuko husababisha uharibifu na ukosefu wa matumaini.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa “Wamarekani wanachochea uharibifu na wanataka kuona Iran iliyoangamizwa badala ya Iran yenye nguvu”. Amesisitiza kuwa Wanataka kuiona Iran ikiwa kama Syria na Afghanistan lakini wamefanya makosa ya kimahesabu, na Wairani shupavu hawatarusu kutokea jambo kama hilo.

4105176

captcha