IQNA

Mgogoro Israel

Hitilafu baina ya mirengo ya kisasa Israel zashadidi zaidi

14:31 - January 22, 2023
Habari ID: 3476445
TEHRAN (IQNA)-Kwa mara nyingine, makumi ya maelfu ya Wazayuni wakazi wa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina na kupachikwa jina la Israel wameandamana dhidi ya serikali yenye misimamo ya kuchupa mipaka ya Benjamin Netanyahu.

Maandamano ya jana Jumamosi yanahesabiwa kuwa makubwa zaidi kuwahi kufanyika mjini Tel Aviv, tangu baada ya Netanyahu kurejea madarakani mwezi uliopita kuongoza baraza la mawaziri lenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia.

Duru za habari zinaarifu kuwa, waandamanaji zaidi ya 100,000 walishiriki kwenye maandamano hayo ya jana ya kulalamikia maamuzi yaliyochukuliwa na serikali ya Netanyahu ya kubana mfumo wa mahakama wa utawala huo.

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa utawala huo haramu, Yair Lapid ni miongoni mwa watu waliojitokeza kushiriki maandamano hayo ya jana Jumamosi mjini Tel Aviv.

Yariv Levin, Waziri wa Sheria katika baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu hivi karibuni aliwasilisha mpango huo kwa ajili ya kufanyia mabadiliko mfumo wa mahakama wa utawala wa Kizayuni; ambapo lengo ni kubana shughuli za mamlaka ya mfumo wa mahakama wa utawala huo. 

Weledi wa mambo wanasema mpango huo unakusudia kuvuruga kanuni ya mgawanyo wa madaraka na kuliongezea uzito bunge na baraza la mawaziri mkabala wa muundo wa mahakama. 

Maandamano ya jana yanaiongezea mashinikizo serikali ya Netanyahu, kwani yamejiri siku chache baada ya Mahakama ya Juu ya Israel kumuagiza Waziri Mkuu huyo kumfuta kazi Aryeh Deri, Waziri wa Mambo ya Ndani anayeongoza chama cha Shas, kwa kupatikana na hatia katika kesi ya uhujumu uchumi.

Ehud Barak, waziri mkuu wa zamani wa utawala wa Tel Aviv ameandika katika makala iliyochapishwa karibuni katika gazeti la Kiibrania la Yedioth Ahronoth kwamba: Hitilafu zilizopo na serikali ya Netanyahu zimefikia kiwango cha vita na hiyo ni indhari ya wazi. Hii ni kwa sababu hatari inakaribia na bila shaka itasambaratisha mfumo wa kisiasa ambao umejengeka juu ya msingi wa kughusubu ardhi za wengine. Matukio mabaya yataendelea kufuatia kuanguka kwa Waisraeli. Kwa hiyo wanapasa kufungua macho yao na kujiuliza wanasimama wapi kwenye mapambano haya, na kisha kujipatia jibu halisi bila kujali litakuwa chungu na zito kiasi gani.

4116147

Kishikizo: israel netanyahu
captcha