IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu

Hizbullah yajiunga na nchi za Kiislamu kulaani kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu huko Sweden

16:42 - January 22, 2023
Habari ID: 3476448
TEHRAN (IQNA) - Harakati ya muqawama ya Hizbullah ya Lebanon imejiunga nan chi za Kiislamu duniani kulaani kitendo cha hivi punde zaidi cha kuvunjiwa heshima Qur'ani nchini Sweden (Uswidi), na kusisitiza kuwa kuudhi matukufu ya Umma wa Kiislamu ni jambo lisilokubalika.

Rasmus Paludan kinara wa chama cha mrengo wa kulia kwa jina la "Stram Kurs" au 'Msimamo Mkali' jana alichoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu karibu na ubalozi wa Uturuki mjini Stockholm tena huku polisi wakiwa wameimarisha hali ya ulinzi na usalama. Kitendo hicho cha Paludan kimelaaniwa vikali na Waislamu na nchi za Kiislamu; ambapo serikali na Sweden imekosolewa kwa kushindwa kuzuia kitendo hicho cha kuwavunjia heshima Waislamu na matukufu yao.  

Hizbullah katika taarifa yake ilieleza kuwa hatua hii ni sehemu ya mfululizo wa matusi ya fedheha kwa matukufu ya kidini ya Waislamu, ikisema mtu hawezi kukaa kimya mbele ya vitendo hivyo.

Harakati ya Hizbullah imezitaka serikali ya Uswidi kuwajibika kikamilifu kwa kitendo hicho cha jinai na kutaka adhabu kwa wale wanaofanya na kuhakikisha kuwa uhalifu kama huo hautatokea tena.

Vile vile imetoa wito kwa serikali, wanazuoni na taasisi za Kiislamu kukemea hatua hiyo na kuhamasisha maoni ya umma wa dunia kuhusu kuchukuliwa hatua za kurudiwa kwa hatua hizo.

Kituo cha Kiislamu cha Al-Azhar cha Misri pia kimelaani kitendo hicho dhidi ya Qur'ani Tukufu, na kusema ni kitendo cha magaidi wenye mafungamano na mrengo wa kulia wa Uswidi na kwamba serikali ya Uswidi ni mshirika katika uhalifu huo.

Al-Azhar imeitaka jumuiya ya kimataifa, mashirika ya kimataifa na viongozi wa dunia kusimama kukabiliana na majaribio hayo ya kudhoofisha matakatifu ya kidini na kulaani vitendo hivyo vya uhalifu vinavyofanywa kwa jina la uhuru wa kujieleza.

Aidha nchi za eneo zimelaani vikali hatua ya chuki dhidi ya Uislamu ya mwanasiasa mashuhuri mwenye misimamo mikali ya kuvunjia heshima nakala za Qur'ani Tukufu katika mji mkuu wa nchi hiyo wa Uswidi, Stockholm.

Iran, Jordan, Kuwait, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu, na Pakistani ni miongoni mwa nchi ambazo zimetoa taarifa kali kulaani kudhalilishwa kwa maandishi matakatifu ya Kiislamu.

Aidha, Katibu Mkuu wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi (P-GCC) Nayef Falah al-Hajraf alikemea mamlaka ya Uswidi kwa kuruhusu mtu mwenye itikadi kali kuchoma Qur'ani Tukufu mbele ya ubalozi wa Uturuki mjini Stockholm, na kusema kitendo hicho kitachochea hisia za Waislamu duniani kote."

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) Hussein Ibrahim Taha Katibu naye pia amelaani jinai iliyofanywa na baadhi ya wanachama wa mrengo wa kulia wenye misimamo mikali ya kuchoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu huko Sweden.

3482166

captcha