IQNA

Jinai za Israel

Israel kujenga nyumba 18,000 katika vitongoji haramu vya walowezi

22:48 - January 25, 2023
Habari ID: 3476462
TEHRAN (IQNA) - Utawala ghasibu wa Israel unaripotiwa kupanga kujenga nyumba 18,000 zaidi vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokoloniwa na utawala huo huko Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Taarifa zinasema baraza la mawaziri la Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu limeanza kujadili hatua za kuharakisha na kuongeza ujenzi wa makaazi katika Ukingo wa Magharibi, kinyume na sheria za kimataifa.

Netanyahu, waziri wake wa vita Yoav Galant, na waziri wa fedha Bezalel Smotrich walikutana mapema wiki hii ili kukamilisha mchakato huo.

Wakati wa mkutano huo, baadhi ya vipengele vya mipango hiyo vilifichuliwa.

Hatua hizi ni pamoja na kuidhinisha uanzishwaji wa makazi mapya 18,000 katika miezi ijayo na kuunda chombo tofauti ambacho kingeidhinisha ujenzi wa majengo yasiyo ya kuishi, kama vile viwanda, miongoni mwa mambo mengine.

Kuidhinishwa kwa hatua hizo kunaweza kusababisha ongezeko kubwa la jamii walowezi wa Kizayuni katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu katika miaka ijayo.

Mnamo mwezi Disemba, Netanyahu alitoa tamko la kisera kwa upande wa baraza lake la mawaziri linalokuja, akitaja upanuzi wa vitongoji haramu vya utawala huo katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina na kwingineko kuwa kipaumbele cha kwanza.

Baraza la mawaziri, alitangaza, “litaendeleza na kustawisha” makazi haramu katika maeneo yote yanayokaliwa kwa mabavu, yakiwemo maeneo ya “Galilaya, Jangwa la Negev, Miinuko ya Golan, Yudea na Samaria (Ukingo wa Magharibi).”

Utawala bandia wa Israel uliundwa  mwaka 1948 baada ya kukalia kwa mabavu maeneo makubwa ya ardhi za Palestina kwa uungaji mkono wa madola ya magharibi.

Utawala huo haramu ulipora  ardhi nyingi zaidi, yaani Ukingo wa Magharibi, unaojumuisha al-Quds (Jerusalem) Mashariki, Ukanda wa Gaza, na Miinuko ya Golan ya Syria katika vita vya mwaka 1967.

Tangu wakati huo, Tel Aviv imejenga zaidi ya vitongoji haramu 250 kwenye ardhi  hizo zinazokaliwa kwa mabavu na kuweka vizuizi vikali zaidi dhidi ya uhuru wa Wapalestina huko. Hivi sasa Wazayuni kati ya  600,000 na 750,000 wanakalia kwa mabavu ardhi hizo za Palestina katika eneo hiyo.

VItongoji vyote vya walowezi wa Kizayuni ambavyo vimejengwa na utawala wa Israel ni kinyume cha sheria kwa mujibu wa sheria ya kimataifa kutokana na ujenzi wake katika eneo linalokaliwa kwa mabavu. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limelaani ujenzi wa vitongoji hivyo kupitia maazimio kadhaa.

3482215

captcha