IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Licha ya njama, Qur'ani Tukufu inazidi kung'aa kila siku na mustakabali ni wa Uislamu

10:09 - January 26, 2023
Habari ID: 3476465
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa taarifa kufuatia kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika nchi kadhaa za Ulaya na kusisitiza kuwa: "Kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu kiwendawazimu chini ya nara ya 'uhuru wa maoni' ni ishara kuwa uistikbari unalenga Uislamu na Qur'ani Tukufu."

Kwa mujibu wa tovuti taarifa katika akaunti ya Twitter khamenei.ir, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amechapisha taarifa katika ukurasa wake wa Twitter kwa lugha ya Kiarabu  kuhusu kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu katika nchi kadhaa za Ulaya na kuongeza kuwa,  licha ya njama hizo za kiistikkbari, "Qur'an Tukufu inazidi kung'aa kila siku na mustakabali ni wa Uislamu." Aidha ujumbe wa Kiongozi Muadhamu umebainisha kuwa, "Wapenda uhuru wote wa dunia wanapaswa kusimama na Waislamu katika kukabiliana na njama mbovu za matusi na uenezaji chuki."

Jumamosi iliyopita Rasmus Paludan, mwanasiasa mwenye misimamo mikali wa Denmark alichoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu karibu na Ubalozi wa Uturuki mjini Stockholm huku akiwa analindwa na polisi ya Uswidi (Sweden)..

Siku ya Jumapili, Edwin Wagensveld, mwanasiasa wa siasa kali za mrengo wa kulia wa Uholanzi, na kiongozi wa kundi la chuki dhidi ya Uislamu la Pegida, alirarua kurasa za Qur’ani Tukufu huko The Hague, mji mkuu wa Uholanzi. Video ya Wagensveld kwenye Twitter ilionyesha kuwa alichoma kurasa zilizochanwa za Qur’ani Tukufu.

Vitendo hivi vimelaaniwa vikali na Waislamu pamoja na nchi za Kiislamu duniani ambapo serikali za Sweden na Uholanzi zimekosolewa kwa kuunga mkono vitendo hivyo viovu.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Uturuki, Kuwait, UAE, Misri, Qatar, Pakistan, Saudia, Morocco, Indonesia na Jordan, ni kati ya nchi za Kiislamu zilizolaani kitendo hicho cha kuvunjia heshima Qur'ani. Aidha taasisi za Kiislamu kama vile Chuo cha Kiislamu cha Al Azhar na Harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Harakati za Hamas na Jihad Islami za Palestina nazo pia zimelaani kitendo hicho kiovu.

4117338

captcha