IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu barani Ulaya

Rais wa Iran: Kuchoma Qur’ani Tukufu ni tusi kwa Dini za Abrahamu

21:32 - January 26, 2023
Habari ID: 3476468
TEHRAN (IQNA) - Rais wa Iran amekashifu kudharauliwa kwa Qur'ani Tukufu na kusema ni dharau kwa Dini za Abrahamu (Ibrahimu )

 “Leo, wanaodai uhuru na haki za binadamu wanaitukana Qur’ani Tukufu. Hii inaonyesha unyonge wao,” Rais Ebrahim Raisi alisema Alhamisi alipokuwa akihutubia mkutano wa ndani mjini Tehran.

"Kitendo chao ni matusi kwa dini zote za Ibrahimu," alisisitiza.

"Watu hawa wanaotoa madai ya  uwongo kuhusu uhuru wa kujieleza wanakashifu ubinadamu kwa kitendo chao cha kuchukiza," alisema, na kuongeza, "Kwa kweli, hawa wanaodai kutetea haki za binadamu ndio wavunjaji wakubwa wa haki hizi,” amesema akiashiria madai ya mara kwa mara ya nchi za Magharibi kuwa ndio watetezi wa haki za binadamu.

Jumamosi iliyopita Rasmus Paludan, mwanasiasa mwenye misimamo mikali wa Denmark alichoma moto nakala ya Qur'ani Tukufu karibu na Ubalozi wa Uturuki mjini Stockholm huku akiwa analindwa na polisi ya Uswidi (Sweden)..

Siku ya Jumapili, Edwin Wagensveld, mwanasiasa wa siasa kali za mrengo wa kulia wa Uholanzi, na kiongozi wa kundi la chuki dhidi ya Uislamu la Pegida, alirarua kurasa za Qur’ani Tukufu huko The Hague, mji mkuu wa Uholanzi. Video ya Wagensveld kwenye Twitter ilionyesha kuwa alichoma kurasa zilizochanwa za Qur’ani Tukufu.

Vitendo hivi vimelaaniwa vikali na Waislamu pamoja na nchi za Kiislamu duniani ambapo serikali za Sweden na Uholanzi zimekosolewa kwa kuunga mkono vitendo hivyo viovu.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Uturuki, Kuwait, UAE, Misri, Qatar, Pakistan, Saudia, Morocco, Indonesia na Jordan, ni kati ya nchi za Kiislamu zilizolaani kitendo hicho cha kuvunjia heshima Qur'ani. Aidha taasisi za Kiislamu kama vile Chuo cha Kiislamu cha Al Azhar na Harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Harakati za Hamas na Jihad Islami za Palestina nazo pia zimelaani kitendo hicho kiovu.

 4117261

captcha