IQNA

Kiongozi Muadhamu abainisha njia ya kukomesha mgogoro Yemen

19:24 - April 08, 2015
Habari ID: 3108936
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Ali Khamenei amesema katika mazungumzo yake na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki aliyeko safarini hapa nchini kwamba mwamko wa Kiislamu ndiyo sababu kuu ya wasiwasi wa maadui wa Uislamu.

Akizungumza Jumanne jioni mjini Tehran,  Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, aliongeza kuwa  kuwa, tukio kubwa na adhimu la mwamko wa umma wa Kiislamu ndiyo sababu kuu inayowatia wahka na wasiwasi maadui wa Uislamu na huku akiashiria njama za maadui za kukabiliana na tukio hilo kubwa amesisitiza kuwa: Hivi sasa Marekani na Wazayuni wanachekelea wanapoona kuna ugomvi na mizozo ndani ya nchi za Kiislamu na kwamba njia ya kuweza kutatua matatizo yaliyopo ni kushirikiana nchi za Kiislamu na kuchukua hatua zinazofaa za kivitendo katika kutatua matatizo hayo.
Aidha katika mazungumzo hayo Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria manufaa na maslahi ya pamoja ya Iran na Uturuki yanayopatikana kwa kuimarishwa uhusiano wa nchi hizo mbili na kuongeza kuwa: Nguvu za nchi yoyote ile ya Waislamu katika ulimwengu wa Kiislamu kwa hakika ni nguvu za umma mzima wa Kiislamu na kwamba siasa kuu na jumla za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kwamba nchi za Kiislamu ziimarishane na zijiepushe na kudhoofishana. Amesema, kuimarishwa uhusiano wa Iran na Uturuki nako kutasaidia katika kulifikia lengo hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Jambo ambalo tumekuwa tukilisisitizia wakati wote ni kwamba, nchi za Kiislamu hazifaidiki na chochote katika kuitegemea Magharibi na Marekani na leo hii yanaonekana kwa uwazi matunda ya vitendo vya Magharibi katika eneo la Mashariki ya Kati ambayo ni kwa madhara ya Uislamu na eneo hili zima.
Vile vile amegusia matukio ya baadhi ya nchi za eneo la Mashariki ya Kati na vitendo vya kinyama vya makundi ya kigaidi katika nchi za Iraq na Syria na kusema: Kama atatokezea mtu akashindwa kuona mkono wa adui katika matukio hayo, basi mtu huyo atakuwa anajidanganya.
Ayatullah Udhma Khamenei ametilia mkazo uhakika huo na kuashiria namna Marekani na Wazayuni wanavyofurahia hali ya machafuko iliyolikumbwa eneo la Mashariki ya Kati na kuongeza kuwa: Wazayuni na nchi nyingi za Magharibi zikiongozwa na Marekani zinafurahia matukio hayo na hazina nia ya kulikomesha na kulimaliza suala la Daesh.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na matamshi yake kwa kutoa baadhi ya mifano ya vitendo vya kihayawani vya kundi la Daesh na ambavyo ni mara chache vimewahi kutokea kama ambavyo amegusia pia lengo la awali kabisa la kundi la kigaidi la Daesh la kutaka kuuteka na kuudhibiti mji mkuu wa Iraq, Baghdad, na kuuliza swali la kimsingi kwamba ni nani analiunga mkono kifedha na kisilaha kundi hilo?
Ameongeza kuwa: Bila ya shaka yoyote mabeberu hawataki masuala yaliyopo katika enei hili yatatuke, hivyo ni nchi za Kiislamu ndizo zinazopaswa kuchukua maamuzi ya kweli ya kutatua matatizo hayo lakini jambo la kusikitisha ni kuona kuwa hakuna maamuzi ya pamoja na yanayofaa yanayochukuliwa kwa ajilli ya kutatua matatizo hayo.
Ayatullah Udhma Khamenei ametolea mfano masuala ya Yemen akisema kuwa huo ni mfano mwingine wa matatizo mapya katika ulimwengu wa Kiislamu na amesisitiza kuhusu utatuzi wa mgogoro wa Yemen kwa kusema: Msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu kuhusu nchi zote ikiwemo Yemen ni kupinga uingilia ma kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hizo, hivyo kwa mtazamo wetu, njia ya kuweza kutatua mgogoro wa Yemen ni kusimamishwa mashambulizi na uingiliaji wa kigenio dhidi ya wananchi wa nchi hiyo, na kuachiwa wananchi wenyewe wa Yemen waamue kuhusu mustakbali wa nchi yao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja tukio adhimu na kubwa la mwamko wa umma wa Kiislamu na kiu yaliyo nayo mataifa mbali mbali kuhusu Uislamu kuwa ndiyo sababu kuu ya woga na wahka walio nao maadui wa Uislamu na kuongeza kuwa: Maadui wameanzisha shambulio lao la kukabiliana na mwamko huo kwa muda mrefu nyuma na kwamba uhakika mchungu ni kuwa, baadhi ya tawala za nchi za Kislamu zinausaliti umma wa Kiislamu na zinatumia fedha na uwezo wao kumtumikia adui.
Baada ya hapo Ayatullah Udhma Khamenei amegusia hali ya Iraq na huku akiashiria misaada ya Iran kwa wananchi wa Iraq iliyosaidia kuzuia kudhibitiwa nchi hiyo na magaidi na kusema: Iran haikutuma jeshi nchini Iraq, lakini kuna uhusiano wa kihistoria, makini, wa muda mrefu na wa karibu baina ya mataifa mawili ya Iran na Iraq.
Aidha Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameomba dua ya kuweza kupata ulimwengu wa Kiislamu heshima na hadhi yake na amesisitiza kuwa, Iran iko tayari wakati wote kwa ajili ya kubadilishana mawazo na kushauriana kwa lengo la kuyatafutia ufumbuzi masuala ya eneo hili.
Katika mazungumzo hayo yaiyohudhuriwa pia na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amegusia mazungumzo aliyofanya na viongozi wa Iran hapa Tehran na kusema kuwa, katika safari yake hiyo kumezungumzwa masuala yanayozihusu nchi mbili ikiwa ni pamoja na masuala yanayohusiana na uhusiano wa kisiasa na kiuchumi pamoja na masuala ya kieneo.
Vile vile amegusia uhusiano wa Tehran na Ankara katika uwanja wa nishati na kuongeza kuwa: Baraza la Ushirikiano wa Kiuchumi la Iran na Uturuki, tayari limeshaundwa na limewataka mawaziri wa nchi mbili kufuatilia kazi za baraza hilo ili kuweze kufanyika kazi kubwa zaidi za kuwezesha kunawiri zaidi na zaidi mabadilishano ya kiuchumi baina ya nchi mbili na kufikia dola bilioni 30 kwa mwaka.
Vile vile Rais wa Uturuki amesisitizia ulazima wa kutatuliwa matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu na Waislamu wenyewe bila ya kuingiliwa na Magharibi na kuongeza kuwa: Hivi sasa eneo la Mashariki ya Kati limekumbwa na matatizo mengi, hivyo nchi za eneo hili zinapaswa kusaidiana kutatua matatizo hayo na hazipaswi kusubiri msaada wa Magharibi kutatua matatizo hayo.
Rais wa Uturuki pia amesema kuwa, anazilaani jinai zinazofanywa na kundi la kigaidi la Daesh na kusisitiza kwa kusema: Mimi siwahesabu Daesh kuwa ni Waislamu na nimeshachukua msimamo wa wazi dhidi yao.../mh

3105459

captcha