IQNA

Waislamu China wazuiwa kufunga Saum ya Ramadhani

13:00 - June 08, 2016
Habari ID: 3470369
Serikali ya China, kwa mara nyingine, imewaamuru wanafunzi, wafanya kazi wa umma na hata wakaazi wa kawaida katika eneo lenye Waislamu wengi la Xinjiang kutofunga Saum ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Taarifa iliyochapishwa katika tovuti rasmi ya serikali katika mji wa Korla mkoani Xinjiang imesema: "Wanachama (wa chama tawala cha Kikomunisti), makada na wafanyakazi wa umma hawapaswi kufunga Saum ya Ramadhani na pia hawapaswi kushiriki katika harakati za kidini mwezi huu."

Taarifa hiyo imeongeza kuwa: "Katika Mwezi wa Ramadhani, hakuna ruhusa ya kufunga biashara za vyakula na vinywaji."

Aidha, tovuti ya Idara ya elimu katika mji mkuu wa mkoa huo, Urumqi, pia imetoa ilani ambapo wanafunzi na waalimu wa shule zote katika eneo hilo wamepigwa marufuku kufunga saum ya Ramadhani na kuenda misikitini katika kipindi hicho.

Kiongozi wa Waislamu wa Kichina wa Kabila la Uighura aliye uhamishoni amelaani vikali vizingiti hivyo na kusema China inautazama Uislamu wa watu wa kabila la Uighur kuwa ni tishio kwa utawala wake.

Mwaka uliopita wa 2015 pia Waislamu wa eneo hilo la Xinjiang pia walipigwa marufuku kufunga saum ya Ramadhani. Chama tawala cha Kikomunisti cha China kwa miaka kadhaa sasa kimekuwa kikiweka vizingiti vya Saum ya Ramadhani katika mkoa wa Xinjiang ambao wakaazi wake wengi ni Waislamu wa kabila la Uighur.

3460030

captcha