IQNA

Mwanaserere aliyevishwa Hijabu, anayesoma aya za Qur'ani

8:59 - September 07, 2017
Habari ID: 3471162
TEHRAN (IQNA)-Mfanyabiashara wa kike Mfaransa ambaye pia ni mama mzazi, Bi Samira Amarir, kwa muda mrefu alikuwa anatafuta bila mafanikio vitu mbali mbali vya watoto kuchezea, ambavyo vingeimarisha imani ya Kiislamu ya binti yake, hatimaye aliamua kujibunia yeye mwenyewe.

Ubunifu wake umepelekea atengeneze mwanaserere (doll) aliyepewa jina la Jenna aliye na Hijabu na ambaye anaweza kusoma sura nne za Qur'ani Tukufu. Hivi sasa Jenna anauzwa katika maeneo mbali mbali duniani hasa nchi za Kiarabu katika Ghuba ya Uajemi.

"Wakati binti yangu alipokuwa na umri wa miaka miwili, nilikuwa natafuta kitu ambacho angeweza kucheza nacho," anasema Bi.Amarir. "Hapo ilinijia fikra ya kutegeneza mwanaserere ambaye angemuwezesha binti yangu kujifunza Qur'ani Tukufu haraka huku akiwa anacheza."

Mwanaserere Jenna ana vazi kamili la Hijabu, aina ya Abaya, yenye rangi za kuvutia na hivyo binti Mwislamu achezaye naye anaweza kuhisi anafungamna na dini yake au ana utambulisho sawa na wa mama yake.

Bi. Amarir anasema wakati binti yake alipoanza kucheza na mwanaserere Jenna, aliweza kuhifadhi sura fupi za Qur'ani ambazo Jenna alikuwa anazisoma. Hivi sasa Bi. Amarir amehama kutoka makao yake nchini Ufaransa na sasa yuko Umoja wa Falme za Kiarabu kwa lengo la kumuuza mwanaserere huyo katika nchi za Kiislamu hasa katika nchi za Ghuba ya Uajemi kama vile Saudi Arabia, Kuwait, Bahrain na Oman.

Kwa muda mrefu watoto Waislamu wamekuwa wakicheza na wanaserere waliotegenezwa katika nchi za Magharibi ambao huakisi utamaduni na ustaarabu wa Kikristo wa nchi hizo na jambo hilo huwa na taathira hasi za moja kwa moja au zisizo za moja kwa moja kwa watoto Waislamu.

Bi. Amarir anasema anafanya utafiti ili kumboresha mwanaserere Jenna katika siku za usoni.

Mwanaserere aliyevishwa Hijabu, anayesoma aya za Qur'ani

3463854

captcha