IQNA

Niyyah na umuhimu wake

16:34 - April 09, 2022
Habari ID: 3475102
TEHRAN (IQNA)- Niyyah au nia ni msingi muhimu wa ibada katika Uislamu na nukta hii inapata umuhimu mkubwa katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Akizungumzia nukta hiyo katika silsila ya darsa za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Dkt. Sheikh Morteza Agha-Tehrani anasema hakuna chochote kinachoweza kufanyika bila nia. Kwa msingi huo Muislamu anapaswa kunuia kuwa sala, saumu, maisha na kifo chake ni kwa ajili ya Allah SWT na njia yake.

Sheikh Agha-Tehrani anafafanua kuhusu nukta hiyo kwa kuashiria aya ya 169 ya  Suurat An'aam  katika Qur'ani Tukufu isemayo: "Sema: Hakika Sala yangu, na ibada zangu, na uhai wangu, na kufa kwangu, ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote."

Anasema aya hiyo inamhusu Nabii Ibrahim AS ambaye ni miongoni mwa Mitume wa ngazi za juu. Anasema wanasaikolojia wa Kimagharibi wanatilia maanani zaidi tabia za mwanadamu katika hali ambayo kwa mtazamo wa Uislamu tabia ina mahala pake lakini nia pia ina umuhimu.

Kwa mfano iwapo mtu mwenye ulemavu wa machi anataka kuvuka barabara nitamsaidia kwa kumshika mkono na kitendo hicho aghalabu kinatokana na huruma au yamkini kitendo hicho kinatokana na nia ya kutaka kuonekana kuwa mtu mwema na mkarimu mbele ya wengine. Pia yamkini kitendo kama hicho kimetendwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ambaye ananipenda na pia anampenda mja ninayemsaidia. Mwenyezi Mungu ametuamurisha tutende mema na tuwe wakarimu na warehemevu kwa wengine.

Kwa hivyo ni wazi kuwa kile kinachosalia katika amali za kila mtu ni nia aliyokuwa nayo.

3478379

captcha