IQNA

Uislamu na Ukristo

Mazungumzo ya Uislamu na Ukristo yapangwa nchini Zimbabwe

22:20 - February 19, 2023
Habari ID: 3476584
TEHRAN (IQNA) – Mazungumzo ya kidini kati ya Uislamu na Ukristo yanapangwa kufanyika nchini Zimbabwe wiki ijayo.

Kituo cha Utamaduni cha Iran nchini Zimbabwe kitaandaa hafla hiyo kwa ushirikiano na Kituo cha Majadiliano kati ya Dini na Tamaduni katika Shirika la Utamaduni na Mahusiano ya Kiislamu (ICRO) kwa ushirikiano na mashirika ya kidini na ya kielimu ya nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.

Chuo kikuu cha Arrupe Jesuit mjini Harare kitakuwa mwenyeji wa mkutano huo siku ya Ijumaa, Februari 24.

Kikao hicho kitajadili maendeleo ya kijamii na kidini katika kanda na duniani kote, kwa kuzingatia uhusiano kati ya Wakristo na Waislamu nchini Zimbabwe.

Viongozi wakuu wa kidini wa Zimbabwe, wasomi wa vyuo vikuu na wakurugenzi wa taasisi za kidini pamoja na mabalozi wa nchi kadhaa na wanazuoni kutoka Iran watashiriki katika mkutano huo.

Umuhimu wa maadili ya kidini katika kudumisha kuishi pamoja kwa amani miongoni mwa wafuasi wa Ukristo na Uislamu na kukabiliana na changamoto za kijamii na kiuchumi, na ugaidi barani Afrika, ni miongoni mwa mada zitakazojadiliwa katika hafla hiyo ya kielimu.

Zimbabwe ni nchi isiyo na bahari kusini mwa Afrika. Watu wengi ni Wakristo kwani zaidi ya asilimia 80 ya Wazimbabwe milioni 16 wanafuata moja ya madhehebu ya Ukristo. Waislamu ni takriban asilimia moja ya wakazi wa nchi hiyo.

 4122981

captcha