IQNA

Mashindano ya Qur'ani ya Iran

Mashindano ya 39 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Iran yaanza rasmi Tehran

21:41 - February 18, 2023
Habari ID: 3476582
TEHRAN (IQNA) – Mashindano ya 39 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yamefunguliwa rasmi Jumamosi Alasiri mjini Tehran.

Sherehe za ufunguzi zilifanyika sambamba na sikukuu ya Idul Maba’ath (kuashiria kuteuliwa kwa Mtume Muhammad (SAW) kama mjumbe wa mwisho wa Mwenyezi Mungu).

Hafla hiyo ilifanyika katika Ukumbi wa Viongozi wa Tehran na kuhudhuriwa na maafisa wa ngazi za juu wa Iran ambapo pia walihutubu katika hafla hiyo.

Hujjatul Islam Seyed Mehdi Khamoushi, mkuu wa Shirika la Masuala ya Wakfu na Misaada Iran, ambalo limeandaa mashindano hayo, alitoa maelezo kuhusu tukio mashindano ya mwaka huu, akibainisha kuwa haya ni mashindano ya kwanza ambayo yanajumuisha kategoria ya  Tarteel kwa wanawake.

Alisema kuwa jumla ya washiriki 52 kutoka nchi 33 watachuana katika fainali ya mashindano hayo mjini Tehran katika siku kadhaa zijazo.

Sherehe hiyo iliendelea kwa hotuba ya Waziri wa Utamaduni na Miongozo ya Kiislamu Mohammad Mehdi Esmaeili.

Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) Mohammad Baqer Qalibaf pia alihutubu akiwa kiongozi wa ngazi za juu zaidi wa Iran aliyehudhuria ufunguzi wa mashindano hayo ya Qur’ani Tukufu.

Katika hotuba yake, allibainisha kuwa kuelewa dhana zilizomo ndani ya Qur'ani Tukufu na kuzitekeleza kunaweza kuleta ustawi, elimu na maendeleo na maendeleo katika mataifa ya Kiislamu.

"Leo hii, umoja na mshikamano kati ya Waislamu ni muhimu zaidi kuliko kitu kingine chochote," alisisitiza na kuongeza kuwa utawala wa Kizayuni Israel hutekeleza njama za mara kwa mara za kuona hitilafu na migongano kati ya mataifa ya Kiislamu katika eneo la Asia Magharibi.

Sherehe za kufunga mashindano hayo zimepangwa kufanyika Jumatano, Februari 22, huku Rais wa Iran Ebrahim Raeisi akitazamiwa kuhudhuria.

Kategoria za mashindano yamwaka huu ya Qur’ani Tukufu ni pamoja na kuhifadhi, kusoma  pamoja na na tarteel kwa wanaume na kuhifadhi na tarteel kwa wanawake.

Jumla ya wasomaji na wahifadhi wa Qur'ani Tukufu 149 kutoka nchi 80 wakiwemo wanaume 114 na wanawake 35 walishiriki katika duru ya mchujo ambayo ilifanyika kwa njia ya intaneti.

Kauli mbiu ya toleo hili, kama lile lililotangulia, ni "Kitabu Kimoja, Umma Mmoja", jambo ambalo linaashiria Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inalipa umuhimu mkubwa umoja na udugu kati ya mataifa ya Kiislamu.

Shirika la Wakfu na Misaada la Iran kila mwaka huandaa mashindano ya kimataifa ya Qur'ani Tukufu kwa kushirikisha wanaharakati wa Qur'ani Tukufu kutoka nchi mbalimbali.

Mashindano ya kategoria za wanaume yanafanyika mnamo Februari 19-21 kutoka tisa alasiri hadi saa tatu usiku kila siku kwa saa za Tehran au saa nane unusu mchana hadi saa mbili unusu usiku kwa saa za  Afrika Mashariki.

Kategoria za wanawake pia zitafanyika mnamo Februari 19-20 kutoka tatu asubuhi hadi saa sita mchana  kwa saa za Tehran.

Mashindano hayo yataonyeshwa moja kwa moja kwenye Televisheni ya Qur'an' TV na Idhaa ya Qur'ani  ya Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB). Unaweza kuyatizama maonyesho hayo mubashara kwa kubonyeza hapa.

 4122846

captcha