IQNA

Wazayuni wayavunjia heshima makaburi ya Waislamu huko Quds

15:02 - July 15, 2015
Habari ID: 3328606
Baraza la Kizayuni la mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu limepitisha mpango wa kuyavunjia heshima na kuyabomoa makaburi ya Waislamu katika mji huo.

Taasisi ya Waqfu na Mirathi ya al Aqswa imetoa taarifa na kulaani kupasishwa mradi wa ujenzi wa nyumba mpya za makazi katika eneo yalipo makaburi ya Waislamu, na kusema kuwa makaburi hayo yataendelea kuwa ya Waislamu, licha ya njama za Wazayuni za kuangamiza utamaduni na historia ya Kiislamu na ya Kiarabu ya Palestina. Duru za habari za Kizayuni zimetangaza habari ya kupasishwa hivi majuzi mradi wa kujenga nyumba mpya za makazi ya walowezi wa Kiyahudi katika eneo yalipo makaburi hayo ya kihistoria katika mji mtukufu wa Quds. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kamati ya kieneo inayohusika na ujenzi na uratibu mipango ya Israel imepasisha mpango wa  kujenga nyumba mpya za makazi 192, hoteli moja na kituo cha biashara katika eneo hilo ambalo kwa mamia ya miaka sasa limekuwa na makaburi ya Waislamu wa mji wa Quds.

Makaburi hayo yaliyo na umri wa miaka 1000 ni urithi wa kiutamaduni wa mji wa Quds na ni ya Wapalestina, na yapo karibu na makaburi ya kihistoria ya Ma’man Allah. Meya wa mji wa Quds unaokaliwa kwa mabavu, miaka kadhaa iliyopita alijenga jumba la makumbusho katika eneo yalipo makaburi hayo licha ya malalamiko makubwa ya wakazi wa Kipalestina wa mji huo mtukufu. Kabla ya hapo pia, meya wa utawala wa Kizayuni huko Quds inayokaliwa kwa mabavu aliratibu na kutekeleza mradi wa kubadili sehemu mojawapo ya makaburi ya Babul- Rahma huko mashariki mwa msikiti wa al Aqswa na kuifanya kuwa bustani. Makaburi ya Babul-Rahma ni moja ya maeneo ya kihistoria ya Quds yenye umri wa miaka 1400 na moja ya milango 12 ya msikiti wa al Aqswa. Taasisi za Kiyahudi zinafanya kila ziwezalo kutekeleza miradi hiyo iliyotajwa huko Baitul Muqaddas inayokaliwa kwa mabavu kwa kuungwa mkono na kushirikiana na mahakama kuu ya Israel. Utawala wa Kizayuni umekuwa ukiwachochea Wazayuni wenye misimamo mikali kucheza na kupiga miguu juu ya makaburi hayo ya Waislamu katika eneo hilo lenye makaburi ya kihistoria. Siasa za kubomoa makaburi ya kihistoria ya Waislamu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, zimekuwa zikitekelezwa tangu huko nyuma na viongozi wa utawala wa Kizayuni. Kitendo cha Wazayuni cha kubomoa makaburi 350 katika eneo yalipo makaburi ya Kiislamu ya Ma’man Allah na kuyavunja ya shakhsia watajika wa Kiislamu, kimekabiliwa na radiamali kadhaa za jamii ya kimataifa khususan kutoka kwa Unesco. Baitul Muqaddas ni eneo linalokaliwa kwa mabavu na Israel  tokea mwaka 1967 wakati wa Vita vya Siku Sita vya mwezi Juni na kwa mujibu wa hati za Umoja wa Mataifa, utawala wa Kizayuni hauna haki ya kulighusubu kivyovyote eneo hilo. Huku Quds Tukufu ikiwa inapitisha miaka 48 ya kukaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni, si tu kuwa utawala huo umebomoa na kuharibu athari za kihistoria za mji huo, bali umejenga na kupanua pia vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina, kuwapatia makazi wahajiri katika vitongoji hivyo na hivyo kuwafukuza majumbani mwao na kuwafanya wakimbizi raia madhlumu wa Palestina. Katika mazingira hayo, Taasisi ya Waqfu na Mirathi ya al Aqswa imeyataka mashirika ya kiutamaduni ya Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa kuchukua hatua haraka iwezekanavyo kuuzuia utawala wa Kizayuni kuendelea kubomoa athari na urithi wa kiutamaduni wa Palestina na wa mji wa Baitul Muqaddas..../mh

3327934

captcha