IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Mwaka mpya ni mwaka wa Uchumi Ngangari, Hatua na Vitendo

15:59 - March 20, 2016
Habari ID: 3470206
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ujumbe wa kuanza mwaka mpya wa 1395 Hijria Shamsia akiwapa mkono wa kheri ya mwaka mpya na Nairuzi wananchi wote na Wairani hususan familia tukufu za mashahidi na majeruhi wa vita.
Mwaka mpya ni mwaka wa Uchumi Ngangari, Hatua na Vitendo
Vilevile amewakumbuka na kuwaenzi mashahidi na Imam Khomeini na kusema: "Mwaka mpya ninaupa jina la Mwaka wa Uchumi Ngangari (kimuqawama), Hatua na Vitendo”.
Ayatullah Khamenei ameashiria suala la kusadifiana siku ya kuzaliwa Bibi Fatima Zahra (as) na mwanzo na mwisho mwaka mpya 1395 na kusema anatarajia kuwa mwaka huu utakuwa mwaka wenye baraka kwa taifa la Iran na katika mwaka huu tutaweza kupata darsa na somo kutokana na miongozo na maisha ya Bibi huyo adhimu kwa kufaidika na masuala ya kiroho ya mtukufu huyo.
Matini kamili ya ujumbe huo ni kama ifuatavyo:

سم الله الرحمن الرحیم
یا مقلّب القلوب و الابصار، یا مدبّر اللّیل و النّهار، یا محوّل الحول و الاحوال، حوّل حالنا الی احسن الحال
Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu
Ewe Mgeuzaji wa nyoyo na basari! Ewe Mpangiliaji wa Usiku na Mchana!
Ewe Mbadilishaji wa mwaka na hali! Badilisha hali zetu kuwa bora ya hali.
 
Assalaamu alaa Swiddiqat at Twahirah, Faatimatu al Mardhiyyah binti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, amani ya Allah iwe juu yake na Aal zake. Amani iwe juu ya Waliyyullahil A'adham roho zetu ziwe fidia kwake na Mwenyezi Mungu aharakishe faraja yake.
Ninaanza kutumia fursa hii kutoa mkono wa baraka na fanaka kwa familia zote za Kiirani na Wairani walioko katika kila kona ya dunia. Nakutakieni sikukuu iliyojaa baraka wananchi wenzangu azizi. Mkono wangu wa baraka za idi uziendee hasa familia azizi za mashahidi, majeruhi azizi wa kivita na familia zao na watu wote wanaojitolea katika njia ya Mwenyezi Mungu na ninaitumia fursa hii kuwakumbuka kwa wema mashahidi wetu watukufu na Imam wetu azizi.
Mwaka huu mpya ulioanza hivi punde - mwaka 95 - (Hijria Shamsia) umepata baraka za jina la Bibi Fatimatuz Zahra (Salamullahi Alayha) mwanzo wake na mwisho wake. Mwanzo wake mwaka huu umesadifiana na maadhimisho ya kukumbuka kuzaliwa mtukufu huyo kulingana na mwaka wa Hijria Qamaria na mwisho wake pia itakuwa vivyo hivyo. Hivyo ni matumaini yetu Inshaallah mwaka huu wa 1395 (Hijria Shamsia) utakuwa mwaka uliojaa baraka za Bibi Fatimatuz Zahra kwa taifa la Iran na tutaweza kufaidika na kupata somo la kimaanawi kutoka kwa mtukufu huyo, na kustafidi vizuri miongozo ya busara ya mtukufu huyo na maisha ya mtukufu huyo.
Mwaka ulioisha - mwaka 94 - kama ilivyokuwa kwa miaka mingine yote, uliandamana na mambo matamu na machungu pamoja na panda shuka nyingi na hilo ni jambo la kawaida katika maisha. Mwaka huo uliandamana na matukio machungu kuanzisha lile la Mina, hadi matukio matamu kama maandamano makubwa ya Bahman 22 (Februari 11, siku zinapofikia kileleni sherehe za Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran) na hadi kwenye uchaguzi wa tarehe 7 Isfand (Februari 26) na vile vile uzoefu wa JCPOA (makubaliano ya nyuklia baina ya Iran na kundi la 5+1) na pia kuanzia kwenye matumaini yalijitokeza hadi kwenye wasiwasi ulioambatana na jambo hilo. Yote hayo ni miongoni mwa matukio ya mwaka huo, na hiyo ndiyo hali inavyokuwa katika miaka yote.
Miaka na siku za maisha ya mwanadamu huandamana na fursa mbali mbali na pia huwa na vitisho tofauti. Vipaji vyetu vinapaswa vionekane kupitia kutumia vizuri fursa tunazopata na hata vitisho tunavyokumbana navyo, ili kuvigeuza vitisho hivyo kuwa fursa nzuri kwetu. Hivi sasa tumeingia kwenye mwaka 95. Katika mwaka huu, kama ilivyo mara zote, zitakuweko fursa mbali mbali na vitisho pia. Kila mmoja wetu anapaswa kufanya juhudi ya kuhakikisha tunatumia vizuri fursa tutakazopata mwaka huu kwa maana halisi ya neno ili kuifanya nchi yetu ishuhudie tofauti za waziwazi na miaka iliyopita, kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mwaka huu.
Kuna matumaini mbali mbali kuhusu mwaka huu wa 1395. Wakati mtu anapoangalia hali na mambo mbali mbali, anapata matumaini mazuri. Tab'an, inabidi juhudi zifanyike ili kufanikisha kivitendo matumaini hayo. Inabidi kufanyike kazi za usiku na mchana na kufanyike jitihada za kila namna bila ya kusita na wala kukwama sehemu yoyote ile katika juhudi za kufanikisha matumaini hayo. Jambo hasa linalotakiwa ni kuwa, taifa la Iran lihakikishe linafanya mambo ambayo yatalitoa katika hali ya kuathiriwa na vitisho vya maadui na uadui wao. Tunapaswa tuhakikishe kuwa tunajiwekea kinga madhubuti ambayo itatufanya tusidhuriwe na vitisho vya maadui. Yaani tuhakikishe kuwa uwezekano wa kudhuriwa na vitisho hivyo ni wa asilimia sifuri.
Ninavyoamini mimi ni kuwa, suala la uchumi ndilo la kupewa kipaumbele cha kwanza kabisa. Yaani wakati mtu anapoangalia masuala yenye vipaumbele anaona kuwa kati ya vipaumbele vyote hivyo, suala la uchumi ndilo la haraka zaidi na la karibu zaidi. Kama kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu, wananchi na serikali na viongozi wa sekta mbali mbali watafanikiwa kufanya kazi nzuri, kwa njia sahihi na inavyotakiwa katika masuala ya kiuchumi, basi ni matumaini yetu kuwa jambo hilo litaathiri pia katika masuala mengine kama vile ya kijamii, kama vile matatizo ya kijamii, kama vile masuala ya kimaadili na kama vile masuala ya kiutamaduni.
Jambo la muhimu na la kimsingi katika suala la uchumi, ni suala la uzalishaji wa bidhaa za ndani ya nchi; ni suala la kuandaa nafasi za kazi na kuondoa ukosefu wa kazi; ni suala la kuimarisha na kusatawisha uchumi na kupambana na uzorotaji wa kiuchumi; hayo ni masuala ambayo wanakabiliana nayo wananchi; hivi ndivyo vitu ambavyo wananchi wanavihisi na wanavitaka na hata takwimu na matamshi ya viongozi wenyewe nchini yanaonesha kuwa, haya ndiyo matakwa ya wananchi na kwa kwa hakika matakwa hayo ni sahihi na ni ya mahala pake kabisa.
Kama tunataka kutatua tatizo la kuzora uchumi, na ili tuweze kutatua tatizo la uzalishaji wa bidhaa za ndani na tutatue pia suala la ukosefu wa kazi, kama tutataka kudhibiti mambo yote hayo, basi tujue kuwa utatuzi wa masuala yote hayo unapatikana katika majimui ya muqawama wa kiuchumi na katika uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete. Uchumi wa kimuqawama unajumuisha mambo yote hayo. Inawezekana kupambana na ukosefu wa kazi kupitia uchumi wa kimuqawama; inawezekana kupambana na uzorotaji wa uchumi kwa kutumia uchumi wa kimuqawama, kama ambavyo inawezekana pia kupambana na ughali wa maisha; kukabiliana na vitisho vya maadui na kusimama kidete kupitia uchumi huo, inawezekana kuiandalia nchi fursa nyingi na kuzitumia vizuri fursa hizo kwa sharti kwamba tuufanyie kazi uchumi wa kimuqawama na tujitahidi kuufanikisha kivitendo na inavyotakiwa.
Ripoti ambazo wamenipa ndugu zetu serikalini zinaonesha kuwa wamefanya kazi kubwa, lakini yote hayo ni utangulizi tu. Kazi za kuandaa miswada na ajenda za sekta tofauti; hizo ni kazi za utangulizi tu; amma jambo la lazima hapa ni kuendelea kwa kazi hizo, jambo la lazima ni kuchukuliwa hatua na kutekelezwa kivitendo mambo hayo, ili wananchi waweze kuona matunda yake; hili ndilo jukumu letu; na Inshaallah nitalitolea ufafanuzi zaidi suala hilo wakati nitakapozungumza na wananchi wetu azizi wa matabaka tofauti.
Kwa kuzingatia yote hayo nimeona nara na kaulimbiu yetu mwaka huu iwe ni "Uchumi wa Kimuqawama, Hatua na Vitendo." Hii ni njia na baraste iliyonyooka kuelekea kwenye kitu tulichokikusudia. Tab'an sitegemei kuwa hatua na vitendo hivyo vitaweza kumaliza matatizo yote katika kipindi cha mwaka mmoja; lakini nina yakini kwamba kama hatua na vitendo vitafanyika kwa mpangililio mzuri na kwa utekelezaji sahihi, basi matunda na athari ya jambo hilo tutaziona wazi wazi mwishoni mwa mwaka huu. Ninawashukuru watu wote waliofanya juhudi na wanaoendelea kufanya juhudi katika njia hii.
Kwa mara nyingine ninatuma salamu na baraka zangu za idi kwa taifa letu azizi nikimuombea rehema na amani Mtume wetu Muhammad na Aal Muhamad pamoja na Imam Mahdi (Amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake, na roho zetu ziwe fidia kwake).
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
3484210
captcha