IQNA

Kiongozi Muadhamu asalisha Sala ya Maiti ya Luteni Jenerali Soleimani na mashahidi wenzake

14:05 - January 06, 2020
Habari ID: 3472339
TEHRAN (IQNA) – Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu leo asubuhi amesalisha Sala ya Maiti ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC na mashahidi wenzake waliouliwa kigaidi na Marekani nchini Iraq, usiku wa kuamkia Ijumaa ya tarehe 3 Januari 2020.

Mamilioni ya wananchi wa Iran leo wameshiriki kwenye shughuli ya mazishi ya mashahidi hao watukufu.

Aidha sambamba na wananchi wa Iran kushiriki kwa mamilioni katika kuwaaga mashahidi hao wakiongozwa na Luteni Jenerali Qassem Soleimani, wametia saini pia tambara kubwa la kuhimiza kulipizwa kisasi cha kuuawa kidhulma mashahidi hao watukufu.

Miongoni mwa waliohudhuria sala hiyo ya maiti ni Rais Hassan Rouhani wa Iran, Spika wa Bunge la Iran Ali Larijani, Mkuu wa Vyombo vya Mahakama Ibrahim Raisi na Kamanda Mkuu wa IRGC Meja Jenerali Salami.

Baada ya kusaliwa, miili mitoharifu ya mashahidi hao imebebwa na mamilioni ya watu kutoka Meidani ya Inqilab hadi Meidani ya Azadi kwa ajili ya kuelekea katika mji mtakatifu wa Qum na baada ya kuagwa na wananchi wanamapinduzi wa mji huo mtukufu, mashahidi hao watazikwa kesho Jumanne kwenye maeneo tofauti.

Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC, Abu Mahdi al Muhandis, Naibu wa Mkuu wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq al Hashd al Shaabi pamoja na wenzao wengine wanane waliuliwa shahidi usiku wa kuamika Ijumaa tarehe tatu Januari 2020 katika shambulio la anga lililofanywa na jeshi la kigaidi wa Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad, mji mkuu wa Iraq.

Ugaidi huo wa Marekani umeendelea kulaaniwa kimataifa huku wananchi wa Iran wakitaka hatua za kulipiza kisasi zichukuliwe.

 

captcha