IQNA

Baraza la Wawakilishi Marekani lapunguza uwezo wa Trump kuanzisha vita dhidi ya Iran

21:02 - January 10, 2020
Habari ID: 3472360
TEHRAN (IQNA) -Baraza la Wawakilishi la Marekani limepitisha muswada wa kupunguza mamlaka ya rais wa nchi hiyo Donald Trump katika masuala ya vita.

Mpango huo uliopewa jina la 'Azimio la Nguvu za Vita dhidi ya Iran' umepitishwa kwa kura 224 zilizounga mkono dhidi ya 194 zilizoupinga. Kabla ya kupitishwa hapo jana, Rais Donald Trump wa Marekani alikuwa amewataka wawakilishi wa chama chake cha Republican wapige kura za kuupinga mpango huo. Sasa muswada huo utapelekwa katika Baraza la Senate kwa ajili ya kuidhinishwa kuwa sheria.
Siku ya Jumatano, Spika wa Baraza la Wawakilishi Nancy Pelosi alieleza kupitia taarifa kwamba, kufuatia mauaji ya kigaidi ya Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu yaliyofanywa kwa amri ya Trump; na kutokana na kuongezeka hali ya wasiwasi na mivutano katika eneo la Asia Magharibi, baraza hilo litapigia kura mpango ambao endapo utapitishwa, utapunguza mamlaka ya Trump ya kuitumbukiza Marekani kwenye mizozo ya kijeshi.
Katika taarifa yake hiyo, Pelosi alibainisha kuwa: "Ijumaa iliyopita, serikali ya Trump iliwashambulia maafisa waandamizi wa kijeshi wa Iran katika shambulio la kijeshi la kichochezi na lisilo na mlingano."
Bi Pelosi alisisitiza katika taarifa yake hiyo kwamba, hatua hiyo ya Ikulu ya White House ilichukuliwa bila kushauriana na bunge la nchi hiyo la Kongresi na imepelekea kushadidi mivutano na Iran katika eneo la Asia Magharibi.
Taarifa hiyo ya Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani ilitolewa saa kadhaa baada ya maafisa waandamizi wa serikali ya Trump kufanya kila waliloweza ili kutetea na kuhalalisha mauaji ya kigaidi ya Kamanda Soleimani kupitia kikao walichofanya na viongozi wa Kongresi.
Luteni Jenerali Qassem Soleimani, kamanda wa kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na Abu Mahdi Al-Muhandis, Naibu Mkuu wa Jeshi la Kujitolea la Wananchi wa Iraq la Al-Hashdu-Sha'abi pamoja na watu wanane wengine waliuawa shahidi usiku wa manane wa kuamkia Ijumaa iliyopita katika shambulio la kigaidi la anga lililofanywa na majeshi vamizi na ya kigaidi ya Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad nchini Iraq.
Kamanda Soleimani alikuwa ameelekea nchini Iraq kwa mwaliko wa serikali ya nchi hiyo.
Usiku wa kuamkia Jumatano, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilijibu jinai hiyo ya kigaidi ya Marekani kwa kuvishambulia kwa makombora vituo viwili vya kijeshi vya Marekani vilivyoko kwenye mikoa ya Al-Anbar na Arbil nchini Iraq na kuwaangamiza askari magaidi wa Kimarekani wasiopungua 80 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 200.

3870488

captcha