IQNA

Maelfu wakamatwa Morocco baada ya kukiuka sheria ya hali ya hatari kuhusu corona

22:31 - April 13, 2020
Habari ID: 3472662
TEHRAN (IQNA)- Watu zaidi ya 4,300 wamekamatwa nchini Morocco katika kipindi cha siku chache zilizopita baada ya kukiuka sheria ya hali ya hatari ambayo inatekelezwa ili kuzuia kuenea ugonjwa hatari wa corona au COVID-19 katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Tokea kati kati ya mwezi Machi, watu 28,701 wamekamatwa kote Morocco ambapo 15,545 miongoni mwao wamefikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kukiuka sheria ya hali ya hatari.

Adhabu ya kukiuka hali ya hatari katika kipindi cha janga la corona ina adhabu ya kifungo cha hadi miezi mitatu jela au fainia ya hadi dola 130, au adhabu zote mbili kwa pamoja.

Kwa mujibu wa sheria ya hali ya hatari ya Morocco iliyoanza kutekelezwa Machi 19, kila mtu anapaswa kubakia nyumbani isipokuwa wale walio na kibali maalumu cha kutoka nje. Aidha wiki iliyopita wakuu wa Morocco walitangaza kuwa, kuvaa maski ni wajibu katika maeneo ya umma. Wanajeshi na polisi wanalinda doria kote Morocco kwa lengo la kutekeleza sheria hiyo ya hali ya hatari.

Hadi kufikia Aprili 13, watu 1,746 walikuwa wameambukizwa corona nchini Morocco na miongoni mwao 120 wamefariki dunia.

Idadi kubwa ya waathirika wako katika mji mkuu wa kibiashara wa Casablanca na mji mkuu wa kisiasa Rabat. Hivi sasa kunatekelezwa sheria kali za karantini katika maeneo yenye msongamamno mkubwa wa watu katika miji mikubwa nchini humo. Hali ya hatari nchini Morocco imepelekea mamilioni ya Wamorocco kukumbwa na hali mbaya ya kiuchumi kwani wengi nchini humo ni vibarua wa kila siku na hali ya sasa imepelekea wakose chakula cha kila siku. Serikali ya nchi hiyo inasema iko mbioni kuwapa watu masikini chakula cha kila siku na msaada wa kifedha.

3471132

captcha