IQNA

Wanazuoni Mashuhuri wa Kiislamu Duniani /4

Msomi wa kwanza kuandika tafsiri ya Qur’ani Tukufu kwa lugha ya Kifaransa

19:57 - November 04, 2022
Habari ID: 3476035
TEHRAN (IQNA) – Allamah Mohamed Ben Checkroun alikuwa mwanachuoni aliyeandika tafsiri na tarjuma ya kwanza ya uhakika ya Qur’ani Tukufu katika lugha ya Kifaransa katika jildi kumi.

Pia alikuwa mwandishi wa vitabu vingine zaidi ya 30 katika uwanja wa tafsiri ya Qur'ani na historia na fasihi ya Morocco kwa Kiarabu, Kifaransa na Kihispania.

Allamah Mohamed Ben Checkroun alizaliwa Morocco mwaka 1932. Alisoma katika shule ya Qur'ani katika utoto mapema na kisha kuendelea na masomo yake katika shule ya kidini, ambayo mwalimu wake mmoja alikuwa baba yake. Alijifunza Qur’ani, Fiqh, na Tafsiri ya Qur’ani Tukufu pamoja na Kifaransa na Kiarabu.

Pia alipata elimu rasmi katika shule mbalimbali huko Marrakech, Rabat, na Paris. Miongoni mwa mafanikio yake mengi ya elimu ya juu ni shahada ya ya uzamivu  mwaka 1974 katika masomo ya ubinadamu nchini Ufaransa.

Huko Ufaransa, msomi huyo wa Morocco alifundishwa chini ya wataalamu kadhaa wa masomo ya Kiarabu na Kiislamu, kama vile Henri Terrasse, Charles Pellat, na Jacques Berque.

Ben Checkroun kisha alianza kufundisha katika shule za Morocco na baada ya muda kufundisha lugha ya Kiarabu, fasihi na ustaarabu katika vyuo vikuu.

Pia alihudumu katika nyadhifa nyingi nchini mwake na pia katika mashirika ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na waziri wa elimu wa Morocco, mshauri wa wizara ya mambo ya nje, mkurugenzi wa idara ya masuala ya kitamaduni katika wizara ya mambo ya ndani, na mkuu wa idara ya utamaduni katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni  (UNESCO).

Aliandika vitabu katika uwanja wa tafsiri ya Qur'ani na kuutambulisha Uislamu kwa nchi za Magharibi kupitia lugha za Ulaya hususan Kifaransa.

Miongoni mwa maandishi yake mengi juu ya elimu, utamaduni, na bila shaka masomo ya Kiislamu, Ben Chekroun labda alikuwa anajulikana sana kwa tafsiri yake ya Qur’ani Tukufu ya jildi 10 kwa lugha ya Kifaransa na pia tarjuma ya Qur’ani Tukufu kwa Kifaransa.

Ilimchukua miaka kumi kuandika tafsiri hiyo na lengo lake kuu lilikuwa ni kupinga maoni potofu katika nchi za Magharibi kuhusu Quran na Uislamu.

"Qur’ani Tukufu Kwa kuzingatia Mada Zake Tofauti", "Faharasa ya Maana na Misingi ya Qur'ani", "Utangulizi wa Mafunzo ya Qur'ani na Hadithi", na "Kamusi ya Qur'ani kwa Kiarabu, Kifaransa na Kihispania" ni miongoni mwa kazi zake nyingine.

Pia aliandika kitabu kiitwacho “Ibada  Katika Uislamu na Muelekeo wake wa Kisiasa, Kijamii na Kielimu” kwa lugha ya Kifaransa. Katika kitabu hiki analenga kueleza matendo ya ibada ya Kiislamu kutoka katika mitazamo ya kihistoria, imani na kisiasa kwa wasomaji wa Kifaransa.

captcha