IQNA

Shakhsia katika Qur'ani /21

Nabii anayejulikana kwa subira na ujasiri

20:50 - December 19, 2022
Habari ID: 3476274
TEHRAN (IQNA) - Watu wengi hawana subira mbele ya matatizo lakini wanapaswa kujua kwamba Mwenyezi Mungu anaweka magumu kwenye njia ya watu ili kuwajaribu. Nabii Ayub-Amani ya Mwenyezi Mungu Iwe Juu Yake (AS)-ambaye alikuwa ni mwenye kumshukuru Mwenyezi Mungu hata katika hali ngumu sana, anaweza kuwa mfano wa kuigwa katika suala hili.

Ayub (AS) ni miongoni mwa Mitume wa Mwenyezi Mungu ambao walikuwa katika kizazi cha Nabii Ibrahim (AS). Mama yake alikuwa kizazi cha Mtume Lut (AS). Imesemekana kuwa mke wake alikuwa binti wa Yusuf (AS) au binti wa Yakub (AS).

Ayub (AS) aliishi eneo la Sham. Aliwaita Bani Israil kufuatia njia ya Mwenyezi Mungu kwa muda wa miaka 17 lakini hakuna aliyemfuata isipokuwa watatu.

Mwenyezi Mungu alimpa baraka nyingi Ayub (AS) na alikuwa mwenye kushukuru daima. Hili lilisababisha moto wa wivu kuwaka ndani ya moyo wa Shetani na akamwomba Mwenyezi Mungu amruhusu kudhibiti alivyomiliki Ayub. Baada ya hapo Ayub (AS) alipoteza vyote alivyokuwa navyo. Kisha Shetani akapuliza pumzi yenye sumu puani mwake. Matokeo yake Ayub alipatwa na maradhi makali ambayo yalimfunika mwili mzima kwa vidonda na majeraha ya ukoma.

Lakini pamoja na hayo yote, Ayub aliendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu. Baada ya kupita mitihani yote migumu, Mwenyezi Mungu alimtuma Malaika ambaye aligonga eneo la ardhi na chemchemi ya maji ikabubujika. Ayub alioga humo na mara moja akaponywa magonjwa na usumbufu wote.

Baadhi wamerejea Aya ya 41 ya Sura ya Saad isemayo, “Na mkumbuke mja wetu Ayubu alipo mwita Mola wake Mlezi akasema: Kwa hakika Shetani amenifikishia udhia na adhabu,” na kuibua maswali juu ya utakaso na utume wa Ayub, wakibishana kwamba alikuwa chini ya ushawishi wa Shetani. Hata hivyo, wanachuoni wamejibu swali hili, wakibainisha kwamba Shetani alikuwa na udhibiti juu ya mwili wa Ayub  na pia mali na milki zake lakini  sio nafsi na moyo wake.

Jina la Ayub limetajwa mara nne katika Qur'ani Tukufu (Katika Sura Al-Ana’am, An-Nisa, Al-Anbiya, na Saad). Katika Sura hizi, marejeo yamefanywa kwa mababu wa Ayub, utume wake, Mwenyezi Mungu kupokea maombi yake na kuwa huru kutokana na magonjwa na matatizo baada ya kupita mitihani ya Mwenyezi Mungu.

Katika Agano la Kale, moja ya vitabu 39 ni kuhusu Ayub (AS) na hadithi yake ni kama ile iliyotajwa ndani ya Qur'ani Tukufu. Tofauti pekee ni kwamba tofauti na Qur'ani Tukufu inavyozungumza kuhusu subira na ujasiri wa Ayub, katika Agano la Kale anasemekana kutokuwa na subira.

Ayub inasemekana aliishi miaka 200, ikiwa ni pamoja na miaka saba au kumi na minane katika ugonjwa. Alizikwa karibu na chemchemi ya maji ambapo alikuwa ameponywa. Hakuna ushahidi kuhusu mahali kaburi lake lilipo ingawa kuna marejeleo ya maeneo katika nchi tofauti kama Iraq, Lebanon, Palestina, na Oman.

captcha