IQNA

Bunge la Oman lapiga marufuku ushirikiano na utawala wa Kizayuni wa Israel

13:10 - December 28, 2022
Habari ID: 3476320
TEHRAN (IQNA)- Baraza la Ushauri la Oman limeikabidhi Kamati wa Kutunga Sheria na Kulinda Haki ya nchi hiyo; muswada wa marekebisho ya kifungu cha 10 cha sheria ya kuharamisha na kupiga marufuku kushirikiana na utawala wa Kizayuni wa Israel ili upasishwe rasmi.

Yaqoob Bin Mohammed bin Khalifa al Harthi, Naibu Spika wa Baraza la Taifa la Ushauri (Bunge) la Oman amesema, muswada huo unatanua wigo wa kupiga marufuku ushirikiano na utawala wa Kizayuni na kukitia nguvu zaidi kifungu cha sheria kinachotilia mkazo suala la kuhesabiwa kuwa ni uhalifu kushirikiana na Israel. Yaqoob al Harthi  pia amesema, hata hivi sasa sheria hiyo inapiga marufuku kushirikiana kwa namna yoyote ile na utawala wa Kizayuni, ni sawa ushirikiano huo uwe baina ya watu na watu au baina ya taasisi na taasisi.

Mkumbo wa nchi za Kiarabu wa kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni ulianza kushuhudiwa mwaka 2020. Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati), Bahrain, Sudan na Morocco ndizo nchi za Kiarabu ambazo zilitangaza uhusiano wa kawaida na utawala pandikizi wa Kizayuni, mwishoni mwa mwaka 2020.

Nchi ya Oman nayo ilikuwa na maelewano ya namna fulani na utawala wa Kizayuni wa Israel hata kabla ya nchi hizo nne za Kiarabu kutangaza rasmi uhusiano wao na Israel. Mwaka 2018, Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni aliitembelea Oman na kuonana na hayati Sultan Qaboos. Lakini pamoja na hayo, uhusiano wa Muscat na Tel Aviv haujaongezeka katika kipindi cha miaka minne iliyopita. Hivi sasa wabunge wa Oman wametaka kukatwa kikamilifu ushirikiano wa kiuchumi, michezo na kiutamaduni na kupigwa marufuku ushirikiano wa aina yoyote na utawala huo katili.

Hatua hiyo ya Bunge la Oman, ni katika kukamilisha Dikrii ya Kifalme nambari 9/72 ya Oman kuhusu kuususia utawala wa Kizayuni na ambayo ilitolewa na Sultan Qaboos. Dikrii hiyo ya Kifalme inatilia mkazo marufuku ya kuweka mikataba ya aina yoyote ile ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja baina ya taasisi na watu wa Oman na utawala wa Kizayuni wa Israel. Dikrii hiyo imepiga marufuku pia miamala na ushirikiano na mashirika yote ambayo yana manufaa au matawi yao katika arhdi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel.

Hatua ya Baraza la Taifa la Ushauri la Oman inaonesha kuwa, uhusiano wa nchi hiyo na utawala pandikizi unaoikalia kwa mabavu Quds Tukufu, hauendi kwa mujibu wa matakwa ya Israel. Viongozi wa utawala wa Kizayuni walikuwa na ndoto ya kuona vikwazo vya kiuchumi baina ya utawala wa Kizayuni na Oman vinapunguzwa. Lakini Bunge la Oman limethibitisha kivitendo kuwa, uhusiano huo unazidi kuporomoka. Kabla ya hapo pia, Oman ilikataa kuruhusu ndege za utawala wa Kizayuni kutumia anga yake. Mwezi Oktoba mwaka huu, vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vilitangaza kufugwa zaidi ya safari 10 za ndege kutoka ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni kuelekea nchini India kutokana na Oman kukataa kuruhusu ndege hizo kutumia anga yake.

Ukweli ni kuwa hatua hii mpya ya Bunge la Oman ni pigo jingine kwa utawala wa Kizayuni katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni. Mwezi mmoja nyuma, wakati Qatar ilipokuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia la Kandanda, raia wa nchi za Kiarabu walitumia fursa hiyo kutangaza waziwazi chuki na hasira zao kwa utawala katili wa Israel. Raia hao hata wa nchi zilizotangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni walisusia kikamilifu kufanya mahojiano na vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni na walitangaza waziwazi kuwa wanaliunga mkono taifa madhlumu la Palestina. Raia hao walisikika wakisema bayana kuwa, katika dunia hii hakuna nchi iitwayo Israel, bali nchi iliyopo ni Palestina.

3481844

captcha