IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kazi kubwa ya Shahidi Soleimani ilikuwa ni kuimarisha na kuhuisha kambi ya Muqawama

17:17 - January 01, 2023
Habari ID: 3476343
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, miongoni mwa kazi kubwa zilizofanywa na Luteni Jenerali Shahid Qassem Soleimani, aliyekuwa Mkuu wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), ni kuhuisha na kutia nguvu kambi ya muqawama au mapambano.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo wakati alipoonana na familia na wajumbe wa kamati ya kumuenzi mwanamapambano huyo shujaa wa Kiislamu na kusema kuwa: Kamanda Soleimani aliitia nguvu za kimaada na kimaanawi kambi ya muqawama na kuyafanya mapambano yake dhidi ya utawala wa Kizayuni na ubeberu wa Marekani na nchi nyingine za kiistikbari yawe imara zaidi na ya kudumu milele.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia jinsi Wapalestina walivyopiga hatua kubwa katika kupambana na Wazayuni na mafanikio makubwa iliyopata kambi ya muqawama huko Iraq, Syria na Yemen na kuongeza kuwa, Luteni Jenerali Qassem Soleimani alitumia uzoefu aliopata katika vita vya kujihami kutakatifu na ushauri wa wafuasi wake, kuutia nguvu muqawama kwa kutegemea uwezo wa kila nchi husika.

Vile vile amesema, kulishinda zimwi kubwa la Daesh (ISIS) na kusambaratisha misingi yake mingi, ni miongoni mwa kazi muhimu zilizofanywa na kamanda huyo wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Ameongeza kuwa, makundi ya muqawama yenyewe yanaona kuwa yamo kwenye kina cha stratijia za Jamhuri ya Kisilamu na ni mbawa za dini tukufu ya Kisilamu. Amesema: Harakati hiyo itaendelea hivyo hivyo katika mustakbali. 

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ametilia mkazo pia wajibu wa kubakisha hai kumbukumbu za mashahidi wote hususan Luteni Jenerali Qassem Soleimani na kusisitiza kuwa, inabidi vipaji mbalimbali vya kisanii vitumike kwa ajili ya kuwaenzi mashahidi hao na kuzibakisha hai kazi zao. 

Lt. Jenerali Soleimani, ambaye alikuwa kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Naibu Kamanda Jeshi la Kujitolea la Wannachi wa Iraq (PMU) Abu Mahdi al-Muhandis, na wanamapambano wenzao waliuawa katika shambulio la ndege zisizo na rubani za Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad mapema  Januari 3, 2020. Shahidi Soleimani alikuwa ameelekea Iraq kwa mwaliko rasmi wa serikali ya nchi hiyo.

Ikulu ya White House na Pentagon ilitangaza kuwa ilihusika na mauaji hayo ya kigaidi  na kuthibitisha kuwa shambulio hilo lilitekelezwa kwa maelekezo ya Rais wa Marekani wa wakati huo Donald Trump.

Mipango mbalimbali imepangwa kuandaliwa nchini Iran, Iraq na nchi nyingine kadhaa ili kuadhimisha kumbukumbu ya kifo cha kishahidi cha Jenerali Soleimani, al-Muhandi na wanajihadi wenzao.

4111242

 

captcha