IQNA

Shakhsia katika Qur'ani Tukufu /40

Uzair; Nabii aliyefufuliwa Baada ya Miaka 100

15:12 - May 08, 2023
Habari ID: 3476976
TEHRAN (IQNA) – Watu wana maswali mengi kuhusu maisha baada ya kifo, ambayo baadhi yake hayajajibiwa.

Si watu wa kawaida tu wanaofikiria maswali kama hayo. Wajumbe wa Mwenyezi Mungu, ambao ni watu maalum na waliochaguliwa, wanaweza pia kuwa na maswali kuhusu suala hili.

Mtume Uzair (AS), anayejulikana pia kama Ezra, alikuwa mmoja wao. Alikuwa wa ukoo wa Harun (AS), ndugu yake Musa (AS).

Uzair na kaka yake pacha Aziz, walizaliwa katika mji mtakatifu wa al-Quds. Katika baadhi ya vyanzo Uzair ametajwa kama kama Ermia.

Inasemekana alikuwa nabii wa Bani Isra’il na aliishi wakati wa utawala wa wafalme wa Achaemenid katika Uajemi.

Kwa mujibu wa Quran Tukufu na baadhi ya vyanzo vya kihistoria, Uzair alipokuwa mdogo, roho yake ilitenganishwa na mwili wake kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Alikufa na akafufuliwa baada ya miaka 100.

Hii ilitokea alipokuwa akipita katika kijiji ambacho wakazi wake wote walikuwa wamekufa. Akiwa njiani, aliona mifupa ya watu waliokufa na kujiuliza jinsi Mwenyezi Mungu atakavyowafufua wafu. Kwa amri ya Mwenyezi Mungu, alifariki papo hapo na akafufuliwa miaka 100 baadaye. Uzair alifikiri alikuwa amelala kwa siku moja au chini ya siku moja.

Kwa mujibu wa baadhi ya tafsiri za Quran, Uzair ndiye aliyewaokoa Bani Isra’il kutoka miaka 100 ya utumwa na uhamisho na kuwarudisha Palestina kutoka Babeli.

Bukht Nassar (Nebuchadnezzar), dhalimu aliyetawala Babeli na aliwahi kuhambulia al-Quds (Jerusalem), ambapo aliharibu mahekalu ya Kiyahudi, alichoma nakala za Torati, aliwaua wengi wa Bani Isra’il na kuwateka waliosalia na kuwapeleka Babeli. Baada ya Mfalme Cyrus wa Uajemi kuteka Babeli, Uzair alimwomba  amruhusu kuwachukua Bani Isra’il na kuwarudisha al-Quds.

Uzair pia anajulikana kama mfufuaji wa Torati iliyosahauliwa. Torati ilikuwa imechomwa moto wakati wa uharibifu wa al Quds na kusahauliwa. Uzair, ambaye alijua yote kwa moyo, alihuisha Torati. Aliisoma kwa watu na wakaiandika.

Jina la Mtume Uzair limetajwa katika Qur'an mara moja. Imo katika Aya ya 30 ya Surah At-Tawbah: “Na Mayahudi wanasema: Uzair ni mwana wa Mungu. Na Wakristo wanasema: Masihi ni mwana wa Mungu. Hiyo ndiyo kauli yao kwa vinywa vyao. Wanayaiga maneno ya walio kufuru kabla yao. Mwenyezi Mungu awaangamize! Wanageuzwa namna gani hawa!.".

Hadithi ya kifo chake kwa muda wa miaka 100 pia imejadiliwa katika Aya ya 259 ya Sura Al-Baqarah, ingawa jina lake halikutajwa.

Kuna maeneo tofauti yanayosemekana kuwa ni mahali pa kuzikwa Mtume Uzair (AS), ikiwa ni pamoja na Ukingo wa Magharibi wa Palestina, Meysan nchini Iraq, na baadhi ya maeneo nchini Iran.

captcha