IQNA

Qur’ani Tukufu Inasemaje/53

Kufeli na ushindi katika maisha sio mambo ya kudumu

16:53 - June 02, 2023
Habari ID: 3477084
TEHRAN (IQNA) – Tunakabiliana na kushindwa na kupata mafanikio katika maisha lakini ni ya muda mfupi. Kwa hiyo hatupaswi kukasirika wakati kuna kushindwa au kufeli.
Kufeli na ushindi katika maisha sio mambo ya kudumu Qur’ani Tukufu inasema, “Kama yamekupateni majaraha, basi na hao watu wengine yamewapata majaraha mfano wa haya. Na siku za namna hii tunaweletea watu kwa zamu, ili Mwenyezi Mungu awapambanue walio amini na awateuwe miongoni mwenu mashahidi. Na Mwenyezi Mungu hawapendi madhaalimu.” (Aya ya 140 ya Surah Al Imran)

Kwa mujibu wa  Tafsiri ya Qur’ani ya Nemuneh ya Ayatullah Nassir Makarim Shirazi, aya hii inaangazia mojawapo ya Sunnah (sheria) za Mwenyezi Mungu na huo ni ukweli kwamba matukio matamu na machungu maishani si ya kudumu.

Matukio haya yanaletwa kwa watu kwa zamu ili waumini watofautishwe na wale wanaodai kwa uwongo kuwa ni waumini.

Mwishoni mwa aya, imesisitizwa kwamba Mungu hapendi madhalimu.

Kwa mujibu wa Tafsiri ya Noor ya Qur'an ya Ayatullah Muhsin Qar’aati, aya hii inarejea kwenye ukweli, yaani, ikiwa waumini wameteseka katika njia ya kutetea haki, maadui pia wanateseka. Ikiwa waumini wameshindwa leo, adui zao pia wamekabiliwa na kushindwa mahali pengine. Kwa hiyo waumini wasikasirike bali wawe na subira katika matatizo.

Maneno Shahid, na Shuhada katika Qur’ani Tukufu kwa kawaida hurejelea “shahidi” na “mashahidi” lakini hapa, kutokana na Shaan Nuzul , yaani sababu na mahali pa kuteremka aya, ambayo ni sehemu ya vita (Vita vya Uhud) inawezekana kwamba neno Shuhada linaweza kumaanisha mashahidi waliopoteza maisha vitani.

Kwa kuzingatia aya hii, Waislamu wanapaswa kuwa imara na wawe na fikra imara na thabiti mbele ya matatizo:

A-  Nyinyi ndio wa juu mkiwa ni Waumini. (Aya ya 139 ya Surah Al Imran)

B- " Kama yamekupateni majaraha," Maadui zako pia wamejeruhiwa.

C- " Na siku za namna hii tunaweletea watu kwa zamu." Siku hizi za uchungu zitapita.

D- ili Mwenyezi Mungu awapambanue walio amini na awateuwe miongoni mwenu mashahidi.

E- Mungu “ na awateuwe miongoni mwenu mashahidi.”

F- Na Mwenyezi Mungu hawapendi madhaalimu, yaani Mungu hawapendi maadui wa waumini.

Imamu Sadiq (AS) alisema kuhusu aya hii kwamba tangu siku Mwenyezi Mungu alipomuumba Adam, kanuni za kimungu na za kishetani zimekuwa katika vita lakini utawala kamili wa Mwenyezi Mungu utawekwa baada ya ujio wa Imam Mahdi (AS).

Ujumbe wa Aya ya 140 ya Surah Al Imran:

1- Waislamu wawe na subira kuliko makafiri. " basi na hao watu wengine yamewapata majaraha mfano wa haya."

2- Matukio matamu na machungu hayadumu. " Na siku za namna hii tunaweletea watu kwa zamu."

3- Katika vita na katika heka heka za maisha waumini wanatofautishwa na wanafiki. "... ili Mwenyezi Mungu awapambanue walio amini na awateuwe miongoni mwenu mashahidi."

4-Mwenyezi Mungu huwachukua mashahidi miongoni mwenu juu ya kuwa kutomtii kiongozi kunapelekea kushindwa. (Mwenyezi Mungu) “Atawafanya baadhi yenu washuhudie vitendo vya watu.”

captcha