IQNA

Watetezi wa Qur’ani Tukufu

Wakristo wa Uswidi wasaidia kuongeza Ufahamu kuhusu Qur’ani Tukufu, Uislamu

21:10 - August 14, 2023
Habari ID: 3477437
STOCKHOLM (IQNA) - Wakristo katika mji ulio karibu na mji mkuu wa Uswidi wanashirikiana na Waislamu kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu Uislamu na Qur’ani Tukufu.

Katika eneo la Fisksatra, kitongoji tulivu katika manispaa ya Nacka nje kidogo ya Stockholm, Waislamu na Wakristo wameishi pamoja kwa amani kwa miaka mingi.

Pamoja, wameshiriki  “sala za amani,” wakapanga sherehe za kitamaduni, na hata kupanga kujenga nyumba zao za ibada karibu na nyingine.

Mshikamano huo umetatizwa na wimbi la hivi karibuni la mashambulizi dhidi ya Qur’ani Tukufu nchini Uswidi, lakini watu wa Fisksatra wameazimia kushinda changamoto hiyo pamoja.

Mwezi Julai, wanachama wa jumuiya za Kiislamu na Kikristo za Fisksatra walisimama bega kwa bega katika uwanja wa Medborgarplatsen huko Stockholm kupinga kuvunjiwa heshima  Qur’ani Tukufu.

Miongoni mwa waliojitokeza katika mjumuiko wa mshikamano ni Carl Dahlback, kasisi wa parokia ya jumuiya ya Nacka ya Kanisa la Sweden.

"Mjumuiko ulikuwa na hisia ya kipekee. Waislamu wengi walinijia na kunishukuru kwa kushiriki katika maandamano ya kupinga kuchomwa moto kwa Qur’ani Tukufu. Walitaka kupiga picha nami,” ameliambia Shirika la Habari Anadolu.

Jumuiya ya Utamaduni wa Kiislamu ya Uswidi (ICC), shirika la Kiislamu lenye makao yake mjini Stockholm, lilisema mjumuiko huo ulikuwa makubwa zaidi uliyofanyika hadi sasa na kuwapa watu njia ya amani ya kutoa maoni yao.

ICC inapanga shughuli kadhaa za kuongeza ufahamu kuhusu Uislamu na kitabu chake kitakatifu.

Ili kufanikisha shughuli hizo, jumuiya za Kiislamu na Kikristo za Fisksatra zitashirikiana, kulingana na Mohammad Aqib, afisa wa ICC.

"Tutaandaa programu kanisani, ambapo kutakuwa na maombi na visomo vya Qur’ani Tukufu," amebaini.

Kundi hilo pia litasambaza nakala za Qur’ani  Tukufu yenye tafsiri ya Kiswidi, pamoja na video za elimu kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii kuhusu kitabu hicho kitakatifu.

Mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya Qur'an nchini Uswidi na nchi jirani ya Denmark yamelaaniwa vikali na Waislamu kote duniani na kutaka hatua zichukuliwe kukomesha vitendo hivyo.

3484776

Habari zinazohusiana
captcha