Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Habari za Qur'ani IQNA, Waziri wa Awqaf Misri Sheikh Mohammad Mokhtar Gomaa amesema semina hiyo itafanyika Jumanne wiki hii na kuwashirikisha maimamu wa misikiti kutoka maeneo yote ya Misri. Viongozi hao wa Kiislamu watachunguza hatari kubwa ya fikra za kitakfiri ambazo zinaenezwa na wafuasi wa pote la Kiwahabi. Sheikh Mohammad Mokhtar Gomaa amesema wizara yake pia inapanga kuandaa semina 100 katika misikit na vituo vya vijana kote Misri kwa lengo la kubainisha kuhusu hatari ya fikra za kitakfiri katika jamii ya Waislamu. Ameongeza kuwa Misri inahitaji kwa uchache miaka mitano kukabiliana na hatari matakfiri au watu wenye misimamo mikali wanaowakufurisha Waislamu. Aidha amesema watu wasio na utaalamu wa masuala ya Uislamu hawataruhusiwa kutoa hotuba katika misikiti nchini humo. Hivi karibuni Sheikh Nabil Qauq, Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Utendaji la Harakati ya Hizbullah nchini Lebanon alionya kuhusu njama za magaidi wa Kiwahabi nchini humo na kusema: "Ugaidi wa kitakfiri hauna dini na wala si dhehebu bali ni shari kamili na ni shari mutlaki na ni tishio kwa watu wote."