IQNA

'Matukio ya ulimwengu si kwa maslahi ya Marekani'

22:28 - March 21, 2014
Habari ID: 1389136
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, matukio ya ulimwengu yanakwenda kinyume na matakwa ya Marekani.

Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo leo ambayo ni siku ya kwanza ya mwaka mpya wa Kiirani wa 1393 Hijria Shamsia mbele ya mamilioni ya Waislamu waliohudhuria mkutano huo katika haram ya Imam Ridha (AS) mjini Masha'had, kaskazini mashariki mwa Iran na kuongeza kuwa, kile ambacho mabeberu wa dunia hususan Marekani, wamekuwa wakikifanya dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Palestina, Syria, Iraq na Afghanistan, kamwe hakitakuwa na manufaa kwao na wala hawatafikia malengo yao. Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa, daima Marekani imekuwa ikifanya njama za kuibadili Palestina kuwa taifa la Kiyahudi, na kumfanya Mpalestina awe Muislamu au Mkristo asiweze kuishi huko Palestina, lakini hata hivyo njama hizo hazikufanikiwa na zimekuwa ni sawa na kuchora ramani juu ya maji na kwamba, hali hiyo ndiyo itakayowakuta mabeberu hata katika siku za usoni. Aidha amesisitiza kwamba, taifa la Iran linatakiwa kuwa imara lenye nguvu mbele ya maadui. Amesema, ikiwa taifa litakuwa dhaifu basi maadui wanaweza kutumia udhaifu huo kufanya hujuma na udhalilishaji. Aidha ameashiria kuwa, nguvu ya taifa haihusiani tu na maandalizi ya silaha za kivita, bali nguvu za nchi zinapatikana pia kwa kuimarisha na kustafidi vizuri na sekta tatu za uchumi, utamaduni na elimu. Amesisitiza kuwa, ikiwa wananchi wa Iran watashikamana, basi wanaweza kuustawisha uchumi wa taifa lao. Ayatullahil Udhma Khamenei amebainisha kwamba, madola ya kibeberu yalikuwa yakidhani kwamba, vikwazo, lugha za kejeli na zisizo na heshima  zingeweza kulifanya taifa la Iran liachane na matukufu yake na kuongeza kuwa, siasa hizo za mabeberu zimewafanya wananchi wa Iran kuwa na irada na azma zaidi ya kushiriki kwa nguvu kubwa zaidi katika nyuga mbalimbali za Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Vile vile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyakosoa madola ya Magharibi yanayodai kupiginia uhuru wa kujieleza na kubainisha kwamba, madola hayo yanasema uongo kwani katika nchi zao mtu haruhusiwi kuzungumzia hata kidogo suala kama la holocaust.

1389093

Kishikizo: khamenei marekani uhcumi
captcha