IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Iran haitayapigia magoti madola makubwa

22:58 - May 14, 2014
Habari ID: 1406967
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, iwapo taifa la Iran litajikita katika kuimarisha uwezo wa ndani ya nchi, basi Marekani na madola mengine makubwa hayawezi kuthubutu kufanya chochote dhidi ya nchi hii.

Sambamba na kuwadia mwezi 13 Rajab na maadhimisho matukufu ya siku ya kuzaliwa Bwana wa wampwekeshao Mwenyezi Mungu, Imam Ali Alayhis Salaam, maelfu ya watu wa matabaka tofauti hasa wananchi wa mkoa wa Ilam (magharibi mwa Iran) Jumanne hii  wameonana na Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika Husainia ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) mjini Tehran.
Katika mkutano huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa kuadhimisha siku ya kuzaliwa Jemedari wa Waumini Imam Ali Alayhis Salaam na kuashiria baadhi ya fadhail, akrama na matukufu mengi yasiyohesabika ya mtukufu huyo.
Vile vile amebainisha mambo manne muhimu na makuu katika maisha ya Imam Ali AS ikiwa ni pamoja na lengo kuu la mtukufu huyo Alayhis Salaam la wakati wa utawala wake, yaani kufanya jitihada za kudhamini saada, ufanisi na ustawi wa kweli wa mwanadamu sambamba na maendeleo yake ya kimaada na kusisitiza kuwa: Moja ya masomo yanayotolewa na mtukufu huyo kwa ajili ya kudhamini ustawi na ufanisi wa kweli katika jamii, ni wajibu wa kufanya jitihada za kustawisha maisha ya watu na kutatua matatizo yao ya kiuchumi na kwamba lengo hilo hivi sasa linaweza kufanikishwa nchini Iran kwa kuwa na mipango sahihi ya kutumia vizuri uwezo usio na kikomo wa ndani ya nchi na kutegemea vipawa vya vijana wa taifa hili.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Ni katika hali na mazingira kama hayo ndipo nchi yetu itakapoweza kupiga hatua za kimaendeleo katika upande wa masuala ya kimaada, kiroho, kiakhlaki, na katika itibari ya kimataifa, heshima na kujiamini kitaifa pamoja na kujitoa katika majivuno na masimbulizi ya maadui wa nje.
Ayatullah Udhma Khamenei ameianza hotuba yake kwa kugawanya akrama na matukufu yanayoeleweka ya Imam Ali Alayhis Salaam katika mafungu manne: "Matukufu ya Kimaanawi," "Jitihada kubwa na kujitolea muhanga kwake," "silika zake kama mtu binafsi, na za kijamii na kiutawala" na "shabaha za mtukufu huyo kwa ajili ya watu" wakati wa utawala wake.
Amma kuhusu matukufu ya kimaanawi ya Imam Ali Alayhis Salaam amesema: Akrama na matukufu ya kimaanawi ya mtukufu huyo kama vile matukufu yake ya kitawhidi, matukufu yake katika ibada, matukufu yake katika kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na matukufu yake katika ikhlasi, yana kina kirefu mithili ya mkondo mkubwa wa bahari na kwamba hadi hivi sasa vipengee vingi vya matukufu hayo havijajulikana; na maulamaa na watu wakubwa wameshindwa kuvitambua.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia jihadi, jitihada kubwa na kujitolea muhanga Imam Ali Alayhis Salaam tangu alipoingia katika Uislamu na kipindi cha kuweko kwake mjini Makkah, kipindi cha Hijra kuelekea Madina, kipindi cha utawala wa Bwana Mtume Muhammad Swallallahu Alayhi Waalih mjini Madina na kipindi cha baada ya kufariki dunia Bwana Mtume na baadaye kukubali kwake ukhalifa na kuongeza kuwa: Amirul Muuminin Alayhis Salaam katika vipindi vyote hivyo alikuwa kwenye kilele cha kujitolea muhanga na jihadi mbali mbali kiasi kwamba alikuwa akimstaajabisha kila mtu katika mambo hayo.
Ayatullah Udhma Khamenei ametaja moja ya vipengee vya kipekee kabisa vya shakhsia ya Imam Ali Alayhis Salaam kuwa ni silika na mwenendo wake kama mtu binafsi, katika jamii na kama mtawala akiongeza kuwa: Amirul Muuminin Alayhis Salaam licha ya kwamba alikuwa mtawala mkubwa, mwenye nguvu na mwenye nchi kubwa sana yenye utajiri mkubwa, lakini aliishi maisha ya chini kabisa, aliishi katika nyumba yenye thamani ya chini kabisa na isiyo na chochote na alisimama imara katika kupigania haki na kusimamisha uadilifu na utawala wa Mwenyezi Mungu na alikuwa akifanya kazi kubwa sana katika uwanja huo.
Vile vile amekitaja kipengee cha nne katika maisha ya Imam Ali Alayhis Salaam kuwa ni shabaha na lengo lake kuu na tukufu kwa ajili ya wananchi wakati wa utawala wake.
Amesema: Amirul Muuminin Alayhis Salaam alibainisha lengo na shabaha yake kuu kuwa ni kuwapeleka peponi watu na kuwaandalia mazingira mazuri ya kuwa na nafasi kubwa katika uwanja wa kutafakari, wa kiroho na kuwa na nyoyo imara katika maisha yao ya kijamii na kwa hakika hilo ni suala muhimu sana na ndilo jukumu kuu la mtawala wa Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha ameashiria baadhi ya masuala ambayo yanayaweka chini ya alama ya kuuliza majukumu ya utawala wa Kiislamu kwa ajili ya kuwapeleka watu peponi na kusema kuwa: Jukumu kubwa la mtawala wa Kiislamu ni kuwaletea wananchi saada, ustawi na ufanisi wa kweli ambapo tab'an jambo hilo halina maana ya kuwatwisha na kuwabebesha mambo watu kwa lazima bali mtawala anapaswa kuzingatia misukumo ya kimaumbile ya watu ya kupenda saada na ufanisi, na kuyatumia maumbile hayo kama medani ya kutoa msaada, miongozo na kuwasahilishia watu njia ya kufikia kwenye lengo hilo kuu na tukufu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Kama jamii ya Kiislamu itakuwa katika kilele cha ustawi wa kimaada, maendeleo ya kielimu na kiviwanda na uhusiano mzuri sana wa kijamii na heshima na utukufu wa kitaifa na kimataifa, lakini wakati watu wa jamii hiyo watakapofariki dunia wakawa hawakujiandalia akiba nzuri ya kwenda kuwasaidia Siku ya Kiyama; jamii hiyo kamwe haiwezi kusemwa kuwa imeishi katika ufanisi na ustawi wa kweli.
Amesema, moja ya njia za kuandaa mazingira ya kuweza watu kufikia kwenye ufanisi na ustawi wa kweli ni kufanya jitihada za kunyanyuma maisha yao na kung'oa mizizi ya umaskini, ukosefu wa kazi, ufa katika matabaka ya watu na ubaguzi na kusisitiza kuwa: Leo hii na kwa taufiki na baraka za Mwenyezi Mungu, viongozi nchini Iran wanafanya jitihada kubwa za kutatua matatizo ya kiuchumi ya wananchi lakini inabidi kuweko uratibu nzuri wa pamoja baina ya fikra zote na kuainishwe njia sahihi za kufanikisha jukumu hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja utekelezaji wa Siasa Kuu za Uchumi wa Kusimama Kidete na kutegemea vipaji, uwezo na vipawa vya ndani kuwa ni njia sahihi ya kutatua matatizo yaliyopo ya kiuchumi na kusisitiza kwamba: Chemchemu zinazofoka kwa nguvu za maendeleo zimechomoza na kwamba maendeleo ya nyuklia, madawa, seli shina, teknolojia ya Nano na miradi ya kiviwanda na kiulinzi ya Iran ni mifano ya wazi ya uhakika huo.
Ayatullah Udhma Khamenei pia amesema: Ni kwa kuzingatia uhakika na ukweli huo ndipo tutakapoweza kuelewa vyema maneno ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) aliposema: Marekani haiwezi kutufanyia ghalati wala upuuzi wowote.
Ameongeza kuwa: Kama tutautumia ipasavyo uwezo wetu wa kitaifa na kutegemea inavyotakiwa mbinde na nguvu zetu za ndani, Marekani na madola mengine hayataweza kutufanyia upuuzi wowote ule, iwe wa kijeshi au usio wa kijeshi na hawataweza kulikwamisha taifa la Iran katika vikwazo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa: Madola ya kibeberu yanapaswa kutambua kuwa, kamwe hayawezi kulipigisha magoti taifa la Iran kwani taifa la Iran ni taifa hai na vijana wa nchi hii wamo katika kupiga hatua kwenye njia sahihi.
Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia baadhi ya mitazamo finyu na isiyoangalia ukweli wa mambo kuhusu vijana wa Iran na namna mitazamo hiyo inavyozingatia zaidi baadhi ya masuala yasiyo sahihi yaliyopo nchini na kusema kuwa: Masuala makuu yanayolihusu taifa la Iran na vijana wa nchi hii ni masuala ya kupenda dini ya Kiislamu na Qur'ani na masuala ya kimaanawi na kiroho pamoja na masuala ya nchi na utaifa wao na kwamba suala hili halipaswi kudharauliwa na kufumbiwa macho hata kidogo.
Amesema, vijana wa nchi yetu ni vijana wazuri na tunapaswa kufanya juhudi kuhakikisha kuwa vijana wetu wanaendelea kuwa wazuri na wanaendelea kuwemo kwenye njia sahihi na wanakuwa na faida kwa nchi yetu katika mustakbali.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile katika sehemu nyingine ya hotuba yake amezungumzia fakhari nyingi za wananchi wa mkoa wa Ilam pamoja na maulamaa, watu wenye vipaji na wahadhiri wa mkoa huo katika nyakati na vipindi tofauti vya Mapinduzi ya Kiislamu ikiwa ni pamoja na nyakati za vita vya kujihami kutakatifu na amewashukuru sana.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Lutfi, Mwakilishi wa Fakihi Mtawala na Imam wa Ijumaa wa Ilam ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Amirul Muuminin Imam Ali Alayhis Salaam na kusema, wananchi wenye ghera wa mkoa wa Ilam katika nyakati na vipindi vyote vya Mapinduzi ya Kiislamu na nyakati za vita vya kujihami kutakatifu walikuwa ni watu wenye busara kubwa, watiifu kwa Jamhuri ya Kiislamu na wamekuwa wakifanya mambo makubwa ya kujivunia.
Vile vile ameshiria nafasi yenye taathira nzuri ya vijana wa mkoa wa Ilam katika operesheni iliyoleta fakhari kubwa ya "Mimak" wakati wa vita vya kujihami kutakatifu na kuongeza kuwa: Matunda ya ushindi ulio wa kujivunia yalikuwa ni kuandaa uwanja wa kuzidi kupata nguvu wanapambano wa Kiislamu na kuendelea kupatikana ushindi mbali mbali wa baadaye katika vita vya kujihami kutakatifu.
Imam wa Sala ya Ijumaa ya Ilam vile vile amezungumzia uwezo mkubwa ulio nao mkoa huo ikiwa ni pamoja na vyanzo vyenye utajiri mkubwa wa mafuta na gesi pamoja na ardhi yenye rutba na kusema kuwa: Kama katika mwaka huu (wa Kiirani wa 1393 Hijria Shamsia) ambao kaulimbiu yake ni mwaka wa Uchumi na Utamaduni wenye Azma ya Kitaifa na Uongozi na Usimamiaji wa Kijihadi utatumiwa vizuri katika kupanga mipango bora ya kustafidi kadiri inavyowezekana na uwezo mkubwa wa kiuchumi wa mkoa huo, basi mkoa wa Ilam utaweza kuwa kambi kubwa ya kiuchumi nchini Iran.

1406452

Kishikizo: khamenei iran marekani
captcha