IQNA

"Waislamu wa Bulgaria wanazidi kushambuliwa"

15:24 - September 01, 2014
Habari ID: 1445545
Mufti Mkuu wa Bulgaria ametahadharisha juu ya kuongezeka mashambulio yaliyoratibiwa dhidi ya Waislamu na maeneo ya ibada ya Waislamu katika nchi hiyo ya Ulaya.

Shirika la Kimataifa la Habari za Qur'ani (IQNA) limemnukuu Sheikh Mustafa Alish Hadji kupitia mtandao wa habari wa World Bulletin akisema kwamba, mashambulio dhidi ya Waislamu nchini Bulgraia yameongezeka sana katika kipindi cha miaka 25 iliyopita kipindi ambacho kilikwenda sambamba na kusambaratika utawala wa Kikomunisti nchini humo. Mufti Mkuu wa Bulgaria amesema kwamba, katika kipindi hicho takribani matukio 250 ya mashambulio ya kupangwa dhidi ya Waislamu na maeneo ya ibada ya Waislamu yameripotiwa nchini humo. Shambulio la hivi karibuni kabisa lililotokana na chuki dhidi ya Uislamu ni lile lililofanywa dhidi ya msikiti wa kihistoria wa Karaja Pasha, shambulio ambalo lilitekelezwa takribani majuma sita yaliyopita na kundi lenye misimamo mikali la mrengo wa kulia linalojulikana kwa jina la Nevrakop. Katika miaka ya hivi karibuni makundi yenye kufurutu ada nchini Bulgaria yamekuwa yakitoa wito wa kufungwa misikiti yote nchini humo. Mashambulio ya chuki dhidi ya Waislamu yamekuwa yakiongezeka nchini Bulgaria katika hali ambayo, kwa karne kadhaa Waislamu wamekuwa wakiishi nchini humo na wanahesabiwa kuwa ni sehemu ya jamii ya nchi hiyo ya Ulaya. Bulgaria ina wakazi milioni saba na nusu huku milioni moja na nusu wakiwa ni Waislamu. Akthari ya Waislamu wa Bulgaria wana asili ya Uturuki na walihajiri kuelekea nchini humo katika kipindi cha utawala wa Othmania na kwa karne nyingi wamekuwa wakiishi kusini mashariki mwa nchi hiyo.

1444298

Kishikizo: waislamu Bulgaria
captcha