IQNA

Umoja wa Mataifa watoa wito wa misaada Afghanistan

19:17 - August 23, 2021
Habari ID: 3474219
TEHRAN (IQNA)- Mashirika ya Umoja wa Mataifa yametaka kuanzishwa mara moja kwa daraja maalum la safari za ndege la kuwezesha ndege zilizobeba misaada ya kibinadamu kuingia nchini Afghanistan kwa ajili ya utoaji wa msaada endelevu na bila vizuizi.

Mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa ni Shirika la Afya Duniani (WHO) na Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF ambayo yametoa wito huo wakati Uwanja wa ndege wa Kabul ukiwa umefungwa baada ya wanamgambo wa Taliban kushika madaraka ya nchi hiyo ilihali kuna haja ya kusambazwa dawa na vifaa vingine vya matibabu ya mamilioni ya watu ikiwemo zaidi ya watu 300,000 ambao wameyakimbia makazi yao katika kipindi cha miezi miwili iliyopita pekee.

Taarifa ya pamoja ya mashirikia hayo mawili imeeleza kuongezeka kwa mahitaji ya kibinadamu huku uwezo wa kusambaza misaada hiyo ukizidi kupungua. 

Mkurugenzi wa WHO kwa ukanda wa Mashariki na Mediterania Dkt Ahmed Al Mandhari  katika taarifa hiyo amesema, “Kwa siku kadhaa macho yote yameelekea kutazama hali iliyopo katika uwanja wa ndege wa Kabul ambapo zoezi la kuwaondoa wafanyakazi wa kimataifa na wa Afghan walio katika hatari, lakini msaada wa kibinadamu unaowakabili wananchi wengi hautakiwi -na hauwezi kupuuzwa.

Ufisadi wa askari wa Marekani

Imefichuka kuwa, maafisa usalama wa Marekani walioko katika Uwanja wa Ndege wa Kabul nchini Afghanistan wanawaitisha mlungula Waafghani wanaotaka kuondoka katika mji mkuu huo.

Duru za kuaminika zimeripoti kuwa, wanajeshi hao wa Marekani wanaodhibiti Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hamid Karzai mjini Kabul tokea Agosti 15 wanawaitisha raia wa Afghanistan rushwa kati dola 500 hadi 2000, kwa yeyote anayetaka kuondoka nchini humo pasi na sababu yoyote ya msingi.

Katika sakata hilo jipya linalofichua sura isiyo ya kibinadamu ya Marekani, askari hao wa US wanafanya ufisadi huo katika hali ambayo, watu saba walifariki dunia hivi karibuni katika msongamano na mkanyagano wa kujaribu kuingia katika uwanja huo wa ndege mjini Kabul.

Haya yanajiri huku dunia ikiendelea kulaani na kusikitishwa na kitendo cha wanajeshi wa Marekani na wale wa NATO cha kutoa kipaumbele kwa shehena za silaha, mbwa na pombe badala ya kuwatanguliza mbele makumi ya maelfu ya wanawake na watoto wa Kiafghani wanaotaka kuondoka nchini humo.

Kundi la Taliban liliteka na kudhibiti Kabul Jumapili ya tarehe 15 Agosti mara tu baada ya Rais Ashraf Ghani kukimbia nchi. Weledi wa mambo wanasema, kutekwa Kabul kulikuwa na maana ya kufikia tamati uvamizi wa miaka 20 wa Marekani na nchi nyingine za Magharibi huko Afghanistan.

3992530

Kishikizo: marekani afghanistan
captcha