IQNA

Kiongozi wa Hizbullah

Yanayojiri Palestina yatakuwa na taathira kwa mustakbali wa utawala wa Israel

13:00 - April 12, 2022
Habari ID: 3475118
TEHRAN (IQNA)- Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrallah amesema kuwa, wananchi wa Palestina hawatashindwa katika mapambano yao ya ukombozi dhidi ya utawala ghasibu wa Israel.

Akizungumzia matukio ya sasa ya Lebanon na eneo la Magharibi mwa Asia Jumatatu jioni, Katibu Mkuu wa Hizbullah aliwaambia Wazayuni kuwa: "Ikiwa mnadhani kwamba Wapalestina watakata tamaa na kwamba usaliti rasmi wa baadhi ya nchi za Waarabu utawafanya vijana wa Kipalestina walegeze kamba, basi hapana shaka kuwa mko kwenye ndoto."

Sayyid Nasrallah amesisitiza kuwa, yanayojiri huko Palestina yatakuwa na taathira kubwa katika mapambano dhidi ya wavamizi na mustakbali wa utawala ghasibu wa Israel.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya nchini Lebanon amezungumzia vita vya mwaka 1996 kati ya muqawama na utawala wa Kizayuni na kuongeza kuwa, vikosi vya muqawama ndivyo vilivyofanikiwa kumlazimisha adui mlingano wa kutofanya mashambulizi dhidi ya raia.

Akizungumzia makubaliano ya usitishaji vita kwa muda wa miezi miwili huko Yemen, Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema, amefurahishwa na uamuzi huo na kuongeza kuwa, Wayemeni wamefanikiwa kuitwisha jamiii ya kimataifa matakwa yao, na kwamba anatumai usitishaji huo wa mapigano utafungua njia ya kupatikana suluhisho la kisiasa la mgogoro wa Yemen.

Sayyid Nasrallah pia ameashiria Siku ya Kimataifa ya Quds na kuwataka wananchi wa Lebanon na Umma wa Kiislamu kushiriki kikamilifu katika shughuli zinazohusiana na siku hii.

Itakumbukwa kuwa mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hayati Imamu Ruhullah Khomeini aliitangaza Ijumaa ya mwisho ya kila mwezi mtukufu wa Ramadhani kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Quds ili kuwahimiza Waislamu kutetea Palestina na kibla chao cha kwanza, yaani Baitul Muqaddas inayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni.  

4048702

captcha