IQNA

Jinai dhidi ya Waislamu

Uholanzi yaomba radhi kutokana na mauaji ya umati ya Waislamu wa Bosnia

17:01 - July 12, 2022
Habari ID: 3475492
Waziri wa Ulinzi wa Uholanzi Kajsa Ollongren amewaomba msamaha kwa Waislamu wa Bosnia na ameshiriki katika ibada ya kumbukumbu ya 27 ya waathirika wa mauaji ya kimbari ya Srebrenica.

Hata hivyo, maneno aliyotumia waziri wa Uholanzi kuomba radhi yanaonyesha kwamba lengo lake lilikuwa tu  kusafisha jina la  walinda amani wa Umoja wa Mataifa wa Uholanzi kuliko kuomba msamaha. Alidai kwamba wanajeshi wa Uholanzi walifanya kila wawezalo kutimiza malengo yao ya kuwatetea watu wasio na hatia wa Srebrenica. Waziri wa Ulinzi wa Uholanzi alisema kwamba maumivu ya mauaji haya hayatafutika kamwe na akataja: ni Waserbia wa Bosnia waliohusika na maafa hayo na wengi wao walihukumiwa katika mahakama za kimataifa.

Hatahivyo  maneno ya walionusurika katika maafa ya Srebrenica na matokeo ya uchunguzi wa kamati za kutafuta ukweli zilizoundwa baada ya maafa ya Srebrenica yanaonyesha madai ya Waziri wa Ulinzi wa Uholanzi hayana ukweli wowote.

Katika maadhimisho ya miaka 27 ya mauaji ya halaiki ya Srebrenica, makumi ya maelfu ya watu walitembea kilomita mia moja hadi Srebrenica kuwakumbuka wahasiriwa wa moja ya mauaji makubwa zaidi ya kimbari barani Ulaya.

Wakati wa hafla hiyo, mabaki yaliyotambuliwa upya  ya waathirika 50 wa maafa ya Srebrenica walizikwa pamoja na wengine 6,671 kwenye Makaburi ya Kumbukumbu ya Srebrenica.

Julai 11, 1995 ni siku ya aibu na majuto kwa serikali za Ulaya zinazodai ubinadamu. Siku hii, msiba mkubwa wa kibinadamu ulitokea katikati ya Ulaya na serikali za Ulaya zilikuwa zikiitazama tu; Serikali za Ulaya zimekuwa zikijitahidi  kadiri ziwezavyo kuficha na kupuuza janga hili la kibinadamu. Waserbia wabaguzi wa Bosnia walifanya uhalifu mkubwa ya kimbari ya Waislamu wa Bosnia kati ya 1992 na 1995 na kuua makumi ya maelfu ya Waislamu Wabosnia wakiwemo  wanawake, watoto, wanaume na vijana. Srebrenica ni kilele cha uhalifu wa Waserbia wahalifu chini ya uongozi wa watenda jinai Radovan Karadzic na Ratko Mladic na msaada wa dikteta wa Yugoslavia Slobodan Milosevic na kwa uungwaji mkono wa Ufaransa na Uingereza.

Katika miezi ya mwisho ya mauaji ya kimbari ya Waislamu wa Bosnia na katika mwaka wa tatu wa mauaji hayo ya kimbari, Umoja wa Mataifa ulitangaza miji mitatu ya Bosnia na Herzegovina kuwa maeneo salama ili kuwaweka raia Waislamu ili wasishambuliwe na wahalifu makatili. Moja ya miji hii ilikuwa Srebrenica. Walinda amani 400 wa Umoja wa Mataifa wa Uholanzi walikuwa wakiulinda mji Srebrenica. Maelfu ya Wabosnia waliokimbia makazi yao walifika Srebrenica kwa dhana kuwa mji huo ulikuwa salama kwao. Lakini Ratko Mladic, mmoja wa viongozi wa uhalifu wa Waserbia wa Bosnia, aliizingira Srebrenica akiwa na wanajeshi 2,000, bila kujali sheria za kimataifa. Mladic alichukua hatua hiyo wakati walinda amani wa Umoja wa Mataifa wa Uholanzi walikuwa na fursa ya kutosha kuripoti kwa serikali zao na maafisa wa Umoja wa Mataifa na kuomba msaada wa dharura. Ni kwa msingi huo ndio Waziri wa Ulinzi wa Uholanzi akaomba radhi lakini hilo halitoshi kwani kuna haja ya kukiri makosa na kulipa fidia kutokana na jinai hiyo.

4070152

captcha