IQNA

Jinai za Israel

Utawala wa Israel waendeleza mauaji ya kimbari Gaza, waliouawa wapindukia 9,000

18:11 - November 03, 2023
Habari ID: 3477833
TEHRAN (IQNA)- Ikiwa ni katika muendelezo wa mauaji ya raia yanayofanywa na utawala haramu wa Israel, ndege za kivita za utawala huo hivi karibuni zilishambulia kwa mabomu kambi ya wakimbizi ya Jabalia iliyoko kaskazini mwa Ukanda wa Gaza na kuua kwa umati zaidi ya raia mia moja wa Palestina na kujeruhi wengine zaidi ya mia tatu.

Wizara ya Afya ya Palestina ilitangaza jana Alhamisi kwamba raia wapatao 9061 wameuawa shahidi, elfu 32 wamejeruhiwa na wengine 2,030 hawajulikani waliko tangu kuanza kwa mashambulizi ya jinai ya Wazayuni katika Ukanda wa Gaza tarehe 7 Oktoba. Imesema thuluthi mbili ya waliouawa shihidi ni wanawake na watoto.

Uchunguzi kuhusu hatua za kijeshi za utawala wa Kizayuni unaonyesha kuwa utawala huo umeweka mauaji ya raia wa kawaida katika ajenda yake. Utawala huo hivi karibuni pia ulishambulia kwa mabomu hospitali ya al-Maamadani huko Gaza, na kuua kwa makusudi Wapalestina wasiopungua 500 na kujeruhi wengine zaidi ya 600.

Kinachofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza ni mfano wa wazi wa jinai za kivita. Ni kutokana na ukweli huo ndio maana jamii ya kimataifa ikakasirishwa sana na uhalifu huo wa kivita na kutaka utawala wa Kizayuni uchukuliwe hatua za kisheria mara moja. Nchi kama Chile na Colombia zimewaita nyumbani mabalozi wao kutoka mjini Tel Aviv, na Bolivia nayo imetangaza kukata kabisa uhusiano wa kidiplomasia na utawala huo wa kibaguzi.

Marekani inaunga mkono jinai za Israel

Suala jingine muhimu linalopasa kuzingatiwa ni kwamba utawala wa Kizayuni unafanya jinai hizo zote dhidi ya Gaza kwa uungaji mkono wa moja kwa moja wa Marekani. Marekani pamoja na nchi mbili za Ufaransa na Uingereza hadi sasa zimezuia kupitishwa azimio lolote dhidi ya jinai za utawala wa Kizayuni katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Dalili nyingine ya uungaji mkono wa Marekani kwa jinai za utawala wa Kizayuni ni kwamba, serikali ya Washington imetangaza rasmi kuwa inapinga usitishaji vita wowote katika Ukanda wa Gaza katika hali ya hivi sasa, kwa sababu usitishaji vita huo hautaunufaisha utawala wa Kizayuni.

Nukta nyingine ni kuwa, mara tu baada ya utawala wa Kizayuni kushambulia kinyama kambi ya wakimbizi ya Jabalia kaskazini mwa Gaza, Anthony Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, alitangaza kwamba atazitembelea ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel kwa mara ya tatu baada ya kuanza vita, ili kuonyesha uungaji mkono wa Marekani kwa utawala huo. Safari hizo zinaonyesha wazi kuwa usimamizi halisi wa vita huko Ghaza uko chini ya serikali ya Marekani.

Yoav Gallant, Waziri wa Vita wa utawala wa mpito wa Kizayuni alijadiliana tena siku ya Jumatano kwa njia ya simu mashambulio dhidi ya Ukanda wa Gaza na Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin. Kwa upande mwingine Isaac Herzog, rais wa utawala wa kigaidi wa Israel pia amezungumza na Anthony Blinken, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kuhusiana na vita hivyo vya kidhalimu vinavyoendeshwa dhidi ya wakazi wa Gaza wasio na ulinzi. Blinken amesema amezungumza na Herzog kuhusu juhudi zinazoendelea za kuwalinda raia wa Marekani na kuwaachia huru wafungwa wa Kizayuni.

Mtamshi hayo na unyama unaofanywa na Israel katika vita hivyo unaonyesha wazi kwamba Wamarekani na pia baadhi ya nchi za Ulaya zinahusika moja kwa moja katika mauaji ya halaiki ya watu wa Gaza. Kwa maneno mengine ni kuwa nchi hizo ni washirika wa jinai zinazofanywa na utawala wa kibaguzi wa Israel dhidi ya raia wa kawaida wasio na hatia, hasa wanawake na watoto. Kuhusiana na hilo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema hivi karibuni katika hadhara ya wanafunzi kwamba: "Ulimwengu wa Kiislamu usisahau kwamba kuhusu kadhia muhimu ya Gaza, waliosimama wazi kulipiga vita taifa madhulumu la Palestina ni Marekani, Ufaransa na Uingereza."

Habari zinazohusiana
captcha