IQNA

Dunia yaunga mkono Palestina

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa laidhinisha kwa wingi azimio la kusitishwa vita Gaza

20:10 - December 13, 2023
Habari ID: 3478027
IQNA-Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeidhinishwa kwa wingi wa kura azimio linatoa wito wa kusitishwa mapigano mara moja huko Gaza kwa sababu za kibinadamu.

Katika kikao cha dharura cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Ukanda wa Gaza kilichofanyika jioni ya jana Jumanne, nchi 153 kati ya wanachama wote 193 wa Umoja wa Mataifa, zilipiga kura kuunga mkono azimio la kusimamisha mapigano mara moja huko Gaza na kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa "mateka" wote.

Wanachama 10 wa Umoja wa Mataifa walipiga kura ya kupinga azimio hilo na wengine 23 hawakupiga kura, hivyo idadi kubwa ya wanachama wa Umoja wa Mataifa walisimama dhidi ya Marekani na utawala haramu wa Israel.

Jaribio la Marekani na nchi za Magharibi la kubadilisha azimio hilo na kuitambulisha harakati ya Hamas kuwa kundi la kigaidi lilishindwa kwa mara ya pili kutokana na upinzani wa nchi wanachama na kushindwa kupatikana kwa idadi inayotakiwa ya kura.

Uingereza, mshirika muhimu zaidi wa Marekani, na nchi kama vile Ujerumani, Italia, Uholanzi na Ukraine pia zilijiepusha kupiga kura kuhusu azimio hilo.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi za Kiislamu na Kiarabu zimepiga kura ya kuunga mkono azimio la kusimamisha vita mara moja huko Gaza. 

Amir Saeid Iravani, balozi na mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema baada ya kura ya zaidi ya theluthi mbili ya wajumbe 193 wa Umoja wa Mataifa waliounga mkono azimio la kusimamisha vita mara moja huko Ghaza kwamba, jinai zinazofanywa na utawala wa Israel lazima zikabiliwe na jibu madhubuti kutoka kwa jamii ya kimataifa, na upinzani wa wazi wa Marekani dhidi ya usitishaji vita huko Gaza, una maana ya kuhalalisha vita, ukatili na hatimaye mauaji zaidi ya watoto na wanawake wa Ukanda wa Gaza.

Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza jana asubuhi ilitangaza kuwa: "Wazayuni wanashambulia hospitali, madaktari na wauguzi; na karibu majeruhi elfu nane wanahitaji kufanyiwa upasuaji haraka iwezekanavyo." 

Maafisa wa tiba wa Gaza wameeleza kuwa, tangu Oktoba 7 mwaka huu Wapalestina karibu 19,000 wamethibitishwa kuuawa shahidi na zaidi ya wengine 49,229 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya kikatili ya anga na nchi kavu dhidi ya eneo hilo. Idadi kubwa ya waliouawa ni wanawake na watoto huku duru zikibaini kuwa watu 8,000 hawajulikani waliko na inaaminika kuwa wamezikwa kwenye vifusi. Takwimu hizi zinazidi kuongezeka hasa kutokana na kushtadi mashambulizi ya utawala wa Israel kusini mwa Ukanda wa Gaza. 

Mashirika ya misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa yameitaja hali ya Gaza kuwa ya maafa katika kalibu ya mashambulizi ya kinyama ya kila uchao ya utawala wa Kizayuni; na kusema: Nusu ya jamii ya wakazi wa Gaza wanakabiliwa na njaa ambapo gharama ya kila gunia moja la unga wa ngano pia imeongezeka na kufikia dola 95 kufuatia vita katika eneo hilo.  

3486400

Habari zinazohusiana
captcha