IQNA

Jinai za Israel

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lapitisha azimio jingine dhidi ya utawala wa Israel

12:50 - January 01, 2023
Habari ID: 3476338
TEHRAN (IQNA)- Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kwa kupitisha azimio, limetaka maoni ya ushauri ya Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ) kuhusu namna utawala ghasibu wa Israel unavyokiuka haki ya Wapalestina ya kujitawala na kujiainishia hatima yao na utawala.

Katika azimio hilo, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeitaka Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu itoe rai au maoni yake ya kisheria kuhusu hatua za utawala ghasibu wa Israel zenye lengo la kubadilisha muundo kijamii wa mji wa Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na utawala huo, sheria za kibaguzi na mipango ya utawala huo ghasibu dhidi ya Wapalestina pamoja na athari za sera na vitendo vya utawala huo  vamizi katika hadhi ya kisheria ya Palestina.
Moja ya vipengee muhimu zaidi katika azimio hili ni kuomba Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifi itoe hukumu au maoni ya kisheria katika kesi mbili:
1- Taathira za kisheria katikak hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel kuendelea kukiuka haki ya wananchi wa Palestina ya kujitawala. 
2- Hatua ya Israel ya ukaliaji mabavu wa muda mrefu, na unyakuzi wa ardhi za Palestina ambazo zimekuwa zikikaliwa kwa mabavu tangu 1967.
Maoni ya ushauri wa kisheria ya ICJ pia yanapaswa kuashiria ni vipi sera na vitendo vya utawala wa Kizayuni vinaathiri hadhi ya kisheria ya ukaliaji mabavu Palestina na halikadhalika madhara ya kisheria ya hatua za Israel kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.

Katika azimio hili, Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anaombwa kuwasilisha ripoti ya utekelezaji wa azimio hili, ikiwa ni pamoja na marekebisho ya Mkataba wa Nne wa Geneva kuhusu hadhi ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Ripoti hiyo inatakiwa kuwasilishwa katika Mkutano wa 78 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa utakaofanyika Septemba mwaka huu.
Katika upigaji kura, nchi 87 ziliunga mkono  azimio hili, nchi 26 zilipiga kura ya kupinga na nchi 53 hazikupiga kura. Marekani, Kanada, Italia, Australia, Austria, Hungary, Jamhuri ya Czech, Guatemala, Estonia, na Ujerumani ni miongoni mwa nchi zilizopiga kura ya kupinga azimio hili licha ya kujifanya kuunga mkono haki za Wapalestina.
Azimio hili limepitishwa Ijumaa ikiwa ni siku moja tu baada ya kuundwa kwa Baraza jipya la Mawaziri la utawala wa Kizayuni wa Israel, ambalo limetangaza upanuzi wa vitongoji vya walowezi haramu wa Kizayuni kuwa mojawapo ya vipaumbele vyake.
Kuidhinishwa kwa azimio hili kulitokana na mapendekezo ya Kamati ya Nne ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambayo iliidhinisha azimio kama hilo mwezi uliopita kwa kuungwa mkono na nchi 98, huku nchi 17 zikipinga, na nchi 52 zikijizuia kupiga kura.
Katika azimio hilo, Baraza Kuu lilitakiwa kufikisha katika mahakama za kimataifa vitendo vya utawala wa Kizayuni vya kukiuka haki ya kujitawala Wapalestina na kukaliwa kwa mabavu kwa muda mrefu ardhi za Palestina na kuendelea ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.
Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na  Baraza la Usalama pekee ndio wanaweza kuomba moja kwa moja na bila masharti maoni ya ushauri kutoka kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu (ICJ).
Mahakama hiyo ina majaji 15 ambao huchaguliwa na Baraza Kuu na Baraza la Usalama kwa kuzingatia mlingano kijiografia kwa muda wa miaka 9. Majaji hawa huchaguliwa kutoka miongoni mwa watu walio na hadhi ya juu zaidi ya kimaadili na wanaohitimu kushikilia nyadhifa za juu za mahakama katika nchi yao au walio na sifa kubwa katika sheria za kimataifa.

4110833

Habari zinazohusiana
captcha