IQNA

Jinai za Israel

UN: Utawala wa Kizayuni wa Israel Unatumia Njaa kama 'Silaha' dhidi ya Wapalestina

16:27 - January 23, 2024
Habari ID: 3478241
IQNA-Ripota wa Umoja wa Mataifa anasema utawala wa Kizyuni wa Israel unatumia njaa kama silaha dhidi ya watu Wapalestina wa Gaza ambao wanakabiliwa na mgogoro mkubwa wa chakula baada ya miaka ya vikwazo na vita vya sasa vya maangamizi ya umati vinavyotekelezwa na Israel.

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya chakula, Michael Fakhri, alisema kuwa watoto wote walio chini ya umri wa miaka mitano huko Gaza wanakabiliwa na utapiamlo na wako katika hatari ya uharibifu usioweza kurekebishwa kwa ukuaji wao wa kimwili na kiakili.

Fakhri aliiambia Al Jazeera kwamba: "Hatujawahi kuona raia milioni 2.2 wakilazimishwa kukabiliwa na njaa katika kiwango hiki. Hatujawahi kuona kiwango hiki cha njaa kikitumika kama silaha."

Mtaalamu mwingine, Alex De Waal, mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Amani Ulimwenguni katika Shule ya Sheria na Diplomasia ya Fletcher katika Chuo Kikuu cha Tufts nchini Marekani, aliunga mkono maoni ya Fakhri, akibainisha kuwa hatua za Israel ni sawa na "uhalifu wa kivita wa njaa".

Aliiambia Al Jazeera kwamba kasi na ukubwa wa shida ya chakula huko Gaza "haijawahi kutokea" katika historia ya kisasa.

Mgogoro wa chakula huko Gaza unakuja huku kukiwa na ongezeko kubwa la machafuko yanayofanywa na Israel, ambayo yamesababisha vifo vya Wapalestina wasiopungua 65 huko Khan Younis kusini mwa Gaza siku ya Jumatatu.

Hayo yanajiri wakati ambao Mamlaka za Palestina zimetangaza kuwa, jeshi vamizi la utawala wa Kizayuni wa Israel limeua watoto 11,000 na wanawake 7,500 katika Ukanda wa Gaza na kuongeza kuwa jeshi hilo katili limedondosha zaidi ya tani 65,000 za mada za miripuko katika vita vya upande mmoja lilivyoanzisha dhidi ya Wapalestina waliowekewa mzingiro.

Taarifa hiyo iliyotolewa jana Jumatatu imeendelea kueleza kuwa, Wapalestina wapatao 7,000 - asilimia 70 kati yao wakiwa ni wanawake na watoto - bado wako chini ya vifusi au wamepotea kutokana na mashambulizi ya kiholela ya jeshi la Israel.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi punde, takriban watu 25,295 wameuawa na 63,000 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya Israel huko Gaza tangu Oktoba 7.

3486917

Habari zinazohusiana
captcha