IQNA

Wanafunzi Waislamu California Marekani wanaonewa

0:01 - November 02, 2015
Habari ID: 3432361
Wanafunzi Waislamu wanaosoma katika shule za umma au za binafsi zisizokuwa za Waislamu katika jimbo la California nchini Marekani wamefanyiwa uonevu au ubaguzi kwa kiwango cha zaidi ya mara mbili kwa wastani wa kitaifa.

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya uchunguzi iliyotolewa na Baraza la Uhusiano wa Kiislamu Marekani (CAIR). Kwa akali, asilimia 55 ya wanafunzi Waislamu 621 waliohojiwa wamesema, katika mwaka uliopita wa 2014 walifanyiwa uonevu unaotokana na sababu za kidini; imeeleza ripoti ya jumuiya hiyo ya haki za kiraia ya Waislamu. Wanafunzi waliosailiwa katika utafiti uliofanywa na Baraza la Uhusiano wa Kiislamu Marekani waliulizwa masuali kadhaa ikiwemo wanajihisi vipi wanapojitambulisha kuwa ni Waislamu na jinsi wanavyotendewa na mamlaka za skuli wanazosoma pamoja na wanafunzi wenzao. Matokeo ya utafiti huo yameonyesha kuwa ubaguzi dhidi ya Waislamu unaongezeka ikilinganishwa na ripoti kama hiyo iliyotolewa na CAIR katika mwaka 2012. Kwa mujibu wa utafiti huo wanafunzi hao wamekuwa wakiudhiwa kwa maneno kuhusiana na dini yao wanapokuwa skuli, wakiwemo wasichana wanaovaa hijabu ambao wamewahi hata kubughudhiwa kwa kushikwa au kuvutwa mitandio waliyovaa na wanafunzi wenzao. Ripoti ya Baraza la Uhusiano wa Kiislamu Marekani imeongeza kuwa wasichana hao Waislamu wanaovaa hijabu huchukuliwa kama watu ambao hawajelimika au hata kukandamizwa kwa sababu ya kuvaa vazi hilo. Ripoti hiyo mpya imetolewa huku jumuiya nyingi za Kiislamu nchini Marekani zikiripoti kuenea kwa ubaguzi wa kidini dhidi ya Waislamu nchini humo.

3422837

Habari zinazohusiana
Kishikizo: waislamu marekani cair
captcha